Home KITAIFA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA LAWAVUTIA VIJANA WA MWANZA, SHINYANGA KUJIANDIKISHA

DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA LAWAVUTIA VIJANA WA MWANZA, SHINYANGA KUJIANDIKISHA


Mwanza

WAKAZI wa Mikoa ya Mwanza na Shinyanga wamejitokeza kwa wingi katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza Agosti 21 na litaendelea hadi Agosti 27,2024 katika mikoa hiyo.

Mwandishi wa habari hii, ameshuhudia uwepo wa wananchi wengi vituoni haswa vijana na wanawake waliojitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Akizungumza Agosti,22 2024 na waandishi wa habari wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa zoezi hilo kwa Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari amesema zoezi limeanza vizuri na mwitikio wa wananchi ni mkubwa.

“Zoezi limeanza vizuri ambapo wananchi wamejitokeza, mawakala wapo vituoni na nimebahatika kuzungumza na mawakala, watendaji vituoni na wananchi kwaujumla zoezi linakwenda vizuri,”amesema Jaji Asina.

Aidha, Jaji Asina amesema changamoto zilizojitokeza ni za kawaida na zinatatulika lakini changamoto kubwa ni wananchi wanaofika kuboresha taarifa zao kusahau majina waliyoyatumia awali kujiandikishia namna yanavyoandikwa kwa usahihi, hivyo inapelekea uchelewaji vituoni.

Amesema makundi maalum ya wamama wajawazito, wanaonyonyesha na kufika na watoto wao vituoni, Wazee, Wagonjwa na wenye ulemavu wameendelea kupewa kipaumbele kama ambavyo Tume inasisitiza.

Jaji Asina ambaye alifanikiwa kutembelea baadhi ya vituo katika Majimbo ya Magu, Nyamagana na  Ilemela amesema licha ya mwitikio huo mzuri kwa siku ya kwanza lakini amewashi wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa siku sita zilobaki na wasisubiri siku ya mwisho.

“Niwasihi wananchi wajitokeze katika vituo ili waweze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ambapo katika vituo tumeona vijana wengi, hivyo watumie siku hizi zilizobaki kuboresha taarifa zao na kuajindikisha,”amesema Jaji Asina.

Mjumbe wa Tume, Balozi Omar Ramadhan Mapuri ambaye yupo Mkoani Shinyanga alisema mkoani humo zoezi hilo limeanza vizuri na wananchi wengi wamejitokeza kujiandikisha kwa wingi.

Mawakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Paul Msafiri na Wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Lydya Martin waliopo kituo cha Bulola Mlimani kilichopo eneo la  Zahanati ya Nyerere katika Halmashauri ya Ilemela wamesema zoezi hilo linakwenda vizuri na hakuna changamoto iliyojitokeza.

Aidha, wakala Fatuma Athumani wa CHADEMA aliyopo kituo cha Miembeni A kilichopo eneo la wazi Nyakabungo A katika Halmashauri ya Jijini la Mwanza amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata haki yao kuewa na kadi ya Mpiga Kura.

Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga limeanza leo Agosti 21 hadi Agosti 27,2024 ambapo Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 400,082 kwenye mikoa hiyo.

Mkoani Mwanza wapiga kura wapya 190,131 wataandikishwa huku Shinyanga wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa ni 209,951. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here