Pwani
SERIKALI inatarajia kuanza kutoa elimu ya fedha kupitia Banki Kuu ya Tanzania (BoT) hasa kuanzia watoto wadogo wajifunze umuhimu wa kuweka akiba binafsi ya kipato chao (fedha za kupewa na Wazazi) hadi kufikia hatua ya kuweka benki lengo likiwa ni kujua thamani ya fedha na kuwa na maamuzi sahihi ya fedha wanayopata ikiwa ni pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya mikopo wanayopewa.
Hayo yamesemwa leo Septemba, 25 2024 na Katibu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanawake kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki moja kwa Wanawake uongozi na usimamizi Jumuishi na endelevu kwa wanawake yanayofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha.
Amesema elimu ya fedha ipo chini sana katika jamii yetu hivyo Wanawake ambao ndio walezi Wakuu wa familia waanze kutoa elimu ya fedha kwa watoto wao angali wakiwa bado watoto dogo.
Amesema watoto wafundishwe wakiwa bado wadogo kuweka akiba ya fedha zao wao wenyewe kwani wakifundishwa wakiwa wadogo ni ngumu kubadilika.
Amesema kwasasa elimu ya fedha ni muhimu iwe inaanzia shuleni Ili kuwaandaa vijana kwa kushiriki shughuli za kiuchumi.
“Kwakuwa kwa kawaida elimu ya fedha illikuwa haifundishwi hivyo kupitia Banki kuu serikali inafanya juhudi za makusudi kutoa elimu ya fedha nchini ambapo Banki kuu watakuwa mafunzo mbalimbali ya fedha kuanzia shule za msingi,” amesema.
Beng’i amesema elimu ya fedha bado Iko chini hapa Tanzania hivyo Wazazi pia wanatakiwa kushiriki kuwafundisha watoto kuweka akiba wakiwa bado wadogo.
Katibu huyo amesema Serikali inatengeneza sera kuhakikisha watanzania wanashiriki kiuchumi hivyo elimu ya fedha ikianza kufundishwa mapema kwa watoto walioko shuleni itasaidia kuleta mabadiliko yanayolengwa.
Amesema Serikali imeendelea kufikisha huduma muhimu kwa wananchi ikiwemo umeme, maji na barabara lengo likiwa ni kuwainua kiuchumi kwa kuwapa fursa za kushiriki katika uzalishaji bila vikwazo.
Aidha amewakumbusha wananchi kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa watakaowavusha kimaendeleo huku akisisitiza Wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea.
Beng’i amesema Wanawake ni kati ya kundi linalojiamiani kwa kutumikia mambo mengi kwa wakati mmoja hivyo wanatakiwa kugombea nafasi za uongozi kuendelea kuonyesha umahiri wao wa kufanya shughuli za Malezi na kuongoza kwenye Jamii.
Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia akiwa katika mafunzo hayo alisema katika Jamii wawezeshaji wakubwa ni Wanawake na hiyo imetokana na Malezi wanayoyapata wakiwa bado wadogo na kwamba mafunzo hayo yatazidi kuwaimazirisha na kuwafanya kuwa imara.
Naye Meneja idara ya mafunzo na Ustawi kutoka shule hiyo ya Uongozi Kabula Igambwa amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongezeka kwa utambuzi kwa wanawake viongozi, kuwa na uongozi Shirikishi na wenye ushindani.