Ruvuma
WAKULIMA nchini wamehaswa kutunza fedha pale wanapouza nafaka zao kwa bei nzuri ili soko linaposhuka wawe na hifadhi ya kutosha. Wameelezwa kuwa bei za masoko hazitabiriki hivyo ni muhimu kwa wakulima kuwa makini na rasilimali fedha wanazochuma.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo Septemba, 24 2024 wakati wa mkutano wake wa hadhara katika Shamba la Kahawa la AVIV Tanzania Limited lililopo katika jimbo la Peramiho, Mkoani Ruvuma.
Shamba hilo ni moja ya mashamba 50 ya Kahawa nchini, na ambalo lina ukubwa wa hekari 50,000. AVIV inazalisha Kahawa kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji wa matone (drip irrigation) kwa asilimia 4 hadi 5 ya Kahawa aina ya Arabica inayozalishwa hapa nchini.
“Mwekezaji huyu amekuwa akitushika mkono katika maeneo ya elimu, afya na ata uzalishaji wa miche. Sasa ni kwenda kuongeza tija kwenye uzalishaji wa jamii kwa kuchimba visima kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa Kahawa wa pembezoni mwa shamba hili la AVIV,” amesema Rais Dk. Samia.
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo, AVIV watakuwa wanahamisha ujuzi kwa wakulima ili kuwa na kilimo cha kisasa cha umwagilaiji (skills and technology transfer).
Rais Dk. Samia pia amefurahishwa na AVIV kubuni mazao mengine zaidi ya kahawa, ambayo ni pilipili manga na paprika (pili pili hoho nyekundu iliyosagwa) ambayo tayari kuna soko kubwa kwenye nchi za Bara la Asia.
“Kwa kuwafundisha wakulima hawa wadogo wa pembezoni jinsi ya kulima kisasa na kuhifadhi mazao haya ya kahawa, pilipili manga na paprika, AVIV linakuwa soko la uhakika,” amesema Rais Dk. Samia.
Amemuelekeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa mbegu za kahawa zinazokwenda kwa wakulima ziendane na mradi huu wa AVIV hususan kwa vile Serikali imeanza kutoa ruzuku kwa mbegu za kahawa.
Ameongeza kuwa hii itaenda kuongeza tija kwenye kilimo cha kawaha ambacho uzalishaji wake kwa sasa ni tani 65,000 kwa matarajio ya mauzo ya Dola za Marekani Milioni 150 hadi zaidi 250; ambapo matarajio ya uzalishaji ni hadi kufikia zaidi ya tani 80,000.
Waziri Bashe pia ameelekezwa kuhakikisha minada ya uuzaji wa kahawa uwe na uwazi ili wakulima wanufaike moja kwa moja huku wakipokea malipo yao ndani ya Siku 2 hadi 3. Kuhusu Vyama vya Ushirika, imeelekezwa kuwa vizidi kuwa imara na kuondokana na makato ya kinyemela na ujanja; na kuhakikisha kuna mifumo inayoeleweka kwa maslahi ya wakulima.