Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni imempandisha kizimani mkazi wa Mabwe pande, Shembiu Shekilaghe(38) akikabiliwa na mashtaka ya kutoa taarifa za uongo na kujiwasilisha kama yeye ni Jakaya Mrisho Kikwete huku akijua sio kweli.
Wakili wa Serikali, Salma Jafari alidai hayo hapo leo Septemba, 23 2024 alipokuwa akimsomea mshtakiwa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hawa Magesa mshtakiwa alipofikishwa mahakamani hapo.
Jafari alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 14, huku mashitaka ya kwanza ya pili na tatu yakiwa ni kutoa taarifa za uongo.
Ilidaiwa Septemba 2,2024 mshtakiwa akiwa katika eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa taarifa za uongo kupitia Akaunti ya mtandao wa kijamii ya Facebook yenye jila la Mrisho Jakaya Kikwete akisema;
“Ukiweka akiba ya 49,000 utapata mkopo wa laki tatu marejesho ni Sh 30,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 10,”
Pia ilidaiwa katika tarehe hiyo kupitia akaunti hiyo pia alitoa taarifa ikisema “ukiweka akiba ya 59,000 utapata mkopo wa Shilingi 400, 000 marejesho ni Sh 40,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 10.”
Pia kupitia akaunti hiyo alitoa taarifa ikisema “ Ukiweka akiba ya Shilingi 69,000 utapata mkpo wa laki tano marejesho ni Sh 50,000 kila mwezi kwa miezi 10.”
Ilidaiwa Juni 7,2024 katika eneo la Kigamoni Wilaya ya Temeke Dar es salaam kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook mshtakiwa kwa nia ovu alijiwasilisha kama mama Salma Kikwete mke wa rais mstaafu wa awamu ya nne.
Pia tarehe hiyo na kupitia akaunti iliyosajiliwa kwa jina la Salma Foundation mshtakiwa alitoa taarifa za uongo akisema “Ukiweka akiba 105,000 itapata mkopo wa milioni moja marejesho laki moja kila mwezi kwa miezi 10 na ukiweka 205,000 utapata mkopo wa milioni mbili marejesho laki mbili kila mwezi kwa miezi 10.”
Mashtaka matano ni ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, ilidaiwa kuwa Septemba 3,2024 katika eneo la Mji mpya Mabwepande mshtakiwa alikutwa akitumia namba ya simu iliyosajiliwa kwa majina ya Matias Ngowi, Modesta Marumi, Jane Mhanga, James Zephania na Amini Omary.
Pia mashtaka mengine ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ilidaiwaJulai 31, 2024 kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina la Tatu Sunzula mshtakiwa alijipatia fedha shilingi 49,000 kutoka kwa Albert Atanas kwa kudai atampa mkopo wa Sh 500,000 huku akijua si kweli.
Pia Agosti 17,2024 kupitia namba hiyo hiyo alijipatia fedha kiasi cha shilingi 100,000 kutoka kwa Samson Mwandawila kwa kudai atampatia mkopo wa Sh 800,000 huku akijua si kweli.
Pia Agosti 9, 2024 kupitia namba hiyo alijipatia fedha kiasi cha shilingi 100,000 kutoka kwa Rudi Maduka akidai atampatia mkopo wa Shilingi 1000,000 kupitia taasisi yake ya Jakaya Kikwete foundation.
Baada ya kusomewa mashtaka yake mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo.
Jafari alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusomaa hoja za awali.
Hakimu Magesa aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, mwaka huu kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.
Hata hivyo, mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.