Dar es Salaam
TAKWIMU za Wizara ya Afya zinaonyesha kila mwaka watoto 7500 huzaliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 01 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi mama na mtoto, Dk.Ahmad Makwani wakati wa mbio fupi hizo zimefanyika katika uwanja wa MUHAS Muhimbili ambapo takribani washiriki 1500 kutoka nchini na Mataifa mbalimbali wameshiriki.
“Washiriki napenda kuwaarifu kwamba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 1.5 katika hospitali za Rufaa za Kanda pamoja na MNH, JKCI na MOI ili kuhakikisha kwamba wale wenye mahitaji maalum kama hawa watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa wanapata huduma bora na kwa wakati bila pingamizi la fedha,” amesema Dk. Ahmad
Amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anajali afya za watanzania kwani ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza sekta ya afya.
Aidha ametoa wito wa watanzania kuendelea kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku sio wakati wa Marathon tuu ili kujenga afya bora na afya ya akili.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI) Dk. Lemeri Mchome ameeleza kuwa wameendesha msimu wa nne wa mbio fupi za MOI maarufu kama “MOI Marathon” kwa lengo la kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi na kuzindua kampeni ya kuwafikia watoto wote wanaozaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi nchini.
Amesema mbio hizo ziligawanyika katika sehemu tatu waliokimibia kuanzia kilomita 5, 10 hadi 21 fedha zilizopatikana lengo ni kuwasaidia watoto 300 wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.
“Tangu kuanzishwa kwa mbio hizi ambapo leo tunatimiza miaka minne hadi sasa tumewafanyia upasuaji watoto 6000 na gharama ya matibabu kwa mtoto mmoja ni ni milioni moja na laki mbili na tumesogeza huduma katika mikoa mbalimbali,”amesema Dk.Mchome.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa kwa sasa wazazi walio jifungua watoto hao wanatengwa na hawezi kufika hospitali na aliwaomba wadau kuendelea kujitokeza ili kuwasaidia watoto hao.
“Nimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendeleza huduma katika sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya huduma katika jamii, tunashukuru kwa mageuzi makubwa katika sekta hii ya afya,” amsema.
Ikumbukwe kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameshatoa mchango wa kusaidia matibabu ya watoto mia wa vichwa vikubwa na mgongo wazi, kwa idadi hiyo itafanya kuwa jumla ya watoto mia mbili kufikiwa na huduma ya matibabu ya vichwa vikubwa na mgongo wazi na alielekeza taasisi ya MOI kuendelea kuzijengea uwezo hospitali za Kanda, Mikoa na Wilaya ili huduma kwa watoto hawa zipatikane mapema na kwa urahisi ili kuwapa nafasi ya kukua kama watoto wengine.