Saidina Msangi, na Josephine Majula, Dodoma.
SERIKALI imeeleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala la ulinzi na usalama wa nchi imekuwa ikitoa msamaha wa kodi kwa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo misamaha inayotolewa kupitia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa Agosti 28, 2024 bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande ,lalipokuwa akijibu swali la Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaondoa mzigo wa kodi kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini.
Chande amesema kuwa kwa mwaka 2024/25, Serikali imefanya marekebisho kwenye kipengele cha 18 cha sehemu ya kwanza ya Jedwali la Msamaha wa Kodi ili kujumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumiwa na vyombo vya ulinzi.
‘‘Lengo la hatua hii ni kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,’’amefafanua Chande.
Vile vile, Chande amejibu swali la Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, aliyetaka kujua kwa muda gani Hazina hulipa malipo ya katikati ya mwezi kwa wastaafu kwa mfuko ulioanza mwaka 1992 kwa kuwa hawalipwi kwa wakati.
Chande amesema kuwa Wizara ya Fedha inahusika kulipa michango ya mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSSSF, ZSSF), WCF na NHIF kila mwezi pamoja na malipo ya nyongeza ya pensheni (additional Pension) kwa PSSSF.
‘‘Wizara ya Fedha hulipa pensheni za kila mwezi pamoja na mafao ya hitimisho kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina,’’ amesema.
Pia, Chande amejibu swali la Dk. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuzielekeza Benki za CRDB, NBC na NMB kufungua matawi eneo la Kikatiti linalokua kwa kasi.
Chande amesema kuwa jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya ulinzi na usalama, miundombinu ya barabara, nishati, maji na TEHAMA.
‘‘Katika mchakato wa kufungua tawi jipya la benki, benki husika hufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujiridhisha kama kuna fursa za kibiashara kukidhi gharama za uendeshaji na kutengeneza faida ambapo upembuzi huo huiwezesha benki husika kufanya maamuzi ya kufungua tawi katika eneo husika,’’ amefafanua Chande.
Ameongeza kuwa pamoja na ukweli kwamba CRDB, NBC na NMB hazina matawi Kikatiti, wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma za kibenki kupitia kwa mawakala.