Home KITAIFA BALOZI KOMBO:APRM KUJITATHMINI KATIKA MASUALA YA UTAWALA BORA AFRIKA.

BALOZI KOMBO:APRM KUJITATHMINI KATIKA MASUALA YA UTAWALA BORA AFRIKA.

Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa Mpango wa kujitathmini katika masuala ya Utawala Bora Afrika (APRM-Tanzania) una umuhimu mkubwa katika kutoa taarifa za nchi ambazo zitatumika kuwabainishia wananchi mambo muhimu na makubwa yanayofanyika nchini kwa lengo la kuyatambua na kuelewa umuhimu wake katika kuchagiaza maendeleo.

Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea Ofisi za APRM Tanzania ziliopo katika Jengo la Wizara hiyo jijini Dar-es-salaam kwa lengo la kuzungumza na watendaji wake na kubadilishana mawazo juu ya Mpango huo.

Balozi Kombo amesema kuwa shughuli zinazofanywa na APRM ni kubwa na muhimu kwa nchi, hivyo chombo hiki kinapaswa kuangaliwa vyema kwa kuboreshewa mazingira ya kazi kwavile Taarifa za APRM zinasaidia katika maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na kuisemea Serikali katika miradi mikubwa inayoitekeleza, hivyo atahakikisha kuwa changamoto zilizopo anazifanyia kazi kwa wakati ili APRM iweze kuleta tija kubwa ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taifa la APRM Profesa Hasa Mlawa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mambo mengi na makubwa na chombo pekee cha kuyaandikia mambo hayo na yakaaminika Kimataifa ni APRM kwavile Tathmini zinazofanywa hufuata misingi na taratibu ambazo ni kufanya Tafiti za kitaalamu, kushirikisha wadau katika kutoa maoni na kutotumika kisiasa.

Ameongeza kuwa, Upo umuhimu mkubwa wa kuwa na Baraza la Usimamizia la Taifa la APRM lililokamilika ili Tanzania ikiandaa Taarifa ya Nchi au Taarifa Mahsusi ziweze kukubalika na kuaminika katika uso wa dunia.

Wakati akifanya uwasilishaji kuhusu utendaji kazi, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Bw. Lamau Mpolo, amesema kuwa dhumuni kuu la APRM Tanzania ni kukuza dhana ya Utawala Bora kwa kutekeleza sera, viwango na taratibu zitakazopelekea kuimarika kwa siasa,kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, uhakika wa maendeleo endelevu na kuharakisha mtangamano wa kikanda na Bara zima la Afrika kwa kubainisha maeneo ambayo zinafanya vizuri na kubadilishana uzoefu katika maeneo ambayo yana changamoto kwa kuyaandalia Mpango kazi na kuweza kushuhulikiwa na Sekta husika.

Amesisitiza kuwa zipo hatua kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha ustawi wa wananchi ambazo ni za kujivunia na kutiliwa mfano barani Afrika. Baadhi ya hatua hizo ni Ujenzi wa Barabara na Miundombinu, Uboreshaji wa huduma za jamii ( Elimu na Afya), Maboresho ya Sekta ya Utalii, Maboresho ya Sekta ya Madini, Kuteua kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi; Kuundwa kwa Tume ya Kupitia upya Haki Jinai pamoja na hatua nyingi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali, ambapo yote haya yanahitji kusemewa na chombo pekee kitakachoweza kusema hayo ni APRM Tanzania.

Ziara hiyo ya Waziri, imefuatiwa baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kumteua tarehe 21/07/2024 na kumuapisha tarehe 26/07/2024 kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here