Home KITAIFA MHAMDISI KASEKENYA AHIMIZA KASI UJENZI BARABARA ARUSHA

MHAMDISI KASEKENYA AHIMIZA KASI UJENZI BARABARA ARUSHA

Arusha

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi STECOL COMPANY anayejenga barabara ya Mianzini-Sambasha inayounganisha barabara ya Mianzini -Ngaramtoni juu-Olemringaringa Sambasha zenye urefu wa KM 18 katikati ya jiji la Arusha kuongeza kasi ya ujenzi.

Amesema kukamilika kwa barabara hizo kutaendelea kuongeza tija kwa huduma ya usafiri kwa wananchi na kuendelea kupendezesha jiji hilo maarufu kwa utalii nchini.

“Ongezeni kasi ya ujenzi, zingatieni ubora, wekeni taa na alama za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuwafanya watumia barabara kufurahi kwa kuwa na barabara nzuri za lami na zinazopitika wakati wote,”amesema Mhandisi Kasekenya.

Amewataka wananchi kulinda alama za barabarani zinazowekwa ili kuwaongoza madereva na watumiaji wa barabara ili kuepuka ajali.

Zaidi ya shilingi bilioni 22 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amekagua barabara ya Usa River- Ngarenanyuki hadi Oldonyo Sambu ambayo maandalizi kwaajili ya kuijenga kwa lami yanaendelea na kuutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha madaraja yanayojengwa sasa yanasanifiwa kwa viwango vya barabara ya lami.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi Chilumba Mohamed amesema wamejipanga kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakidhi viwango vya juu vya ubora na hadhi ya jiji la Arusha linalopokea wageni wengi.

” Tutaendelea kutoa elimu ya matumizi bora ya barabara ili kuepusha ajali na kulifanya jiji la Arusha mahali salama pa watu kutalii na kuishi”, amesisitiza Mhandisi Mohamed.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here