Home KITAIFA DK. NCHEMBA AIHAKIKISHIA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUBORESHA MIFUMO Ya KODI.

DK. NCHEMBA AIHAKIKISHIA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUBORESHA MIFUMO Ya KODI.

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali inaendelea kuweka na kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuboresha mifumo yake ya kodi. 

Dk. Nchemba ameyasema hayo leo Agosti 20 2024 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, wakati akiagana na Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake wa ubalozi hapa nchini, Mhe. Didier Chassot.

Amesema kuwa Rais. Samia Suluhu Hassan, ameunda timu ya wataalam ya kupitia na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mifumo yake ya kodi ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini.

Dk. Nchemba amefafanua kuwa pamoja na kuundwa kwa timu hiyo, Serikali pia imechukua hatua kadhaa za kuboresha ya kielektroniki ya ukusanyaji kodi inayosaidia kukusanya mapato yake kwa ufanisi na kuondoa usumbufu kwa walipa kodi.
Alisema kuwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuimarisha mifumo ya kodi ni kuhakikisha kuwa idadi ya walipakodi inaongezeka hatua itakayosaidia pia kuiwezesha Serikali kupunguza viwango vya kodi ya ongezeko la thamani siku za usoni kwa sababi walipakodi watakuwa wengi.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake hapa nchini, Didier Chassot, ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kupitia mifumo ya kodi na kwamba anaamini Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini watapata pia nafasi ya kuzungumza na kujadiliana na Serikali kuhusu masuala hayo kama walivyoomba.

Balozi Chassot alitumia fursa hiyo ya kuagana na Waziri wa Fedha,Dk. Mwigulu Nchemba, kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua kubwa iliyopiga kimaendeleo katika kipindi kifupi.

Ameahidi kuwa Uswisi inaandaa mpango mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, utakaojielekeza katika kufanikisha agenda mbalimbali za maendeleo ya nchi kupitia program zake mbalimbali ikiwemo kusaidia mfuko wa maendeleo ya jamii-TASAF, usimamizi wa fedha za umma, biashara na uwekezaji kupitia asasi za kiraina sekta binafsi.

Didier Chassot, ameitumikia nafasi hiyo ya ubalozi akiwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka minne na ameahidi kuendelea kuwa Balozi mzuri wa Tanzania atakaporejea nchini kwake kuendelea na majukumu yake mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here