Home KITAIFA WIZARA YAAINISHA MIKAKATI YA KUKUZA LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

WIZARA YAAINISHA MIKAKATI YA KUKUZA LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

Dodoma

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dk. Damas Ndumbaro ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuwa, wizara hiyo iko katika utekelezaji wa malengo mahususi ya kuhimiza na kuendeleza matumizi ya lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi, kupitia uanzishaji wa shule ya Kiswahili na Stadi za Kiafrika.

Ndumbaro ameyasema hayo Agosti 19, 2024 Jijini Dodoma akieleza kuwa, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) linaendelea na mipango ya ujenzi wa shule ya Kiswahili na Stadi za Afrika kwa lengo la kuhimiza matumizi na maendeleo ya Kiswahili duniani ambapo amesema, Baraza hilo tayari limeandaa andiko dhana maalumu na kuliwasilisha UNESCO na taratibu za kupata eneo la ujenzi wa shule hiyo zinaendelea vyema.

Amesema matumizi ya Kiswahili yamejikita katika nyanja zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi katika mataifa mbalimbali akibainisha kuwa, matumizi ya lugha hiyo yameongeza idadi ya watumiaji wa Kiswahili ambapo hadi Agosti mwaka 2024 lugha hiyo imefikisha wazungumzaji zaidi ya milioni 500 duniani, ongezeko la watumiaji wa Kiswahili linaenda sambamba na ongezeko la machapisho ya Kiswahili kwa upande wa isimu na fasihi na kumekuwa na chachu kwa waandishi wengi kuanza kuandika kwa Kiswahili.

Dk.Ndumbaro amesema lugha ya Kiswahili inafundishwa katika vituo na vyuo mbalimbali duniani ambapo hadi Agosti, 2024 imefikia vituo na vyuo 150 huku idadi ya Walimu wa kufundisha lugha hiyo waliopelekwa na Serikali nje ya nchi wakifikia 113.

Ameongeza kuwa, lugha ya Kiswahili sasa inatumiwa katika matangazo ya idhaa mbalimbali za redio za kimataifa ambapo hadi kufikia mwezi Agosti 2024 jumla ya redio na televisheni zipatazo 44 zinatumia lugha ya Kiswahili hatua ambayo inakuza, kupanua na kuongeza utambulisho wa Tanzania.

Pia ameeleza kuwa, lugha ya Kiswahili imekuwa lugha ya mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, lugha rasmi na lugha ya kazi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Wazalishaji wa Almasi Afrika hatua ambayo imesababisha kuongezeka kwa huduma za tafsiri na ukalimani.

Aidha, amewaeleza wajumbe hao wa Kamati kuwa, lugha ya Kiswahili imeendelea kupata hadhi kubwa kimataifa kufuatia Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutangaza siku maalumu ya maadhimisho ya Kiswahili ambayo ni Julai 7 ya kila mwaka ambapo Kiswahili kimekuwa lugha ya kwanza ya Afrika kutengewa siku ya maadhimisho ambapo mwaka 2024 yamefanyika kwa mara ya tatu tangu yalipoanza rasmi mwaka 2022.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa, Baraza la Taifa la Kiswahili linaendelea na uundaji wa Kongoo ya Kiswahili ya Taifa ili kuwezesha uendelezaji wa matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kwa njia ya TEHAMA ambapo hadi kufikia Julai, 2024 limeandaa na kupakia kwenye seva maneno 39,000,000 kati ya 50,000,000 yaliyolengwa kuingizwa kwenye kongoo hiyo ambayo itakuwa njia ya kuingia kwenye maandalizi ya akili mnemba katika Kiswahili.

Kwa upande wao wajumbe wa Kamati hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti wameishauri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iangalie namna ya kuanzisha mfumo utakaowezesha lugha ya Kiswahili kuwa ya lazima katika matumizi ya shughuli zote kote nchini kama yanavyofanya mataifa mengine ikiwemo Jamhuri ya Watu wa China ili kuweka msukumo kwa wageni wanaotembea Tanzania kujifunza Kiswahili kama lugha ya lazima katika shughuli mbalimbali zikiwemo za biashara pamoja na kuwatumia watu mashuhuri katika ubidhaishaji wa Kiswahili nje ya nchi.

Aidha, wameishauri Wizara hiyo ishirikiane na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuweka utaratibu wa kuwezesha somo la Kiswahili liwe la lazima na kigezo cha ufaulu wa wanafunzi katika alama za mitihani ya mwisho kama ilivyo kwa somo la Hisabati ili kuongeza msisitizo wa umuhimu wa lugha hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here