Home KITAIFA KASEKENYA TANROADS NA WANANCHI LINDENI BARABARA

KASEKENYA TANROADS NA WANANCHI LINDENI BARABARA

Pwani

NAIBU Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kushirikiana na wananchi kulinda hifadhi za barabara na hivyo kuwezesha ujenzi wa miundombinu hiyo kufanyika kwa urahisi na kudumu kwa muda mrefu.

Akikagua ujenzi wa barabara ya Mkuranga-Kisiju KM 45 na barabara ya Kilwa mkoani Pwani amehimiza ushirikishwaji wa wananchi katika kulinda hifadhi ya barabara ili kuepuka uvamizi wa hifadhi hizo hali inayosababisha uchimbaji wa mchanga na mawe na hivyo kuathiri barabara na madaraja wakati wa mvua.

“TANROADS waelimisheni wananchi ili wazuie wenzao kulima, kujenga na kuchunga mifugo kwenye hifadhi za barabara ili kulinda barabara na kuzikarabati kwa urahisi inapohitajika”, ameelekeza Kasekenya.

Mkoa wa Pwani ni mkoa wa Viwanda hivyo ujenzi na ukarabati wa barabara hizi za Kilwa na Mkuranga-Kisiju KM 45 uzingatie ubora na viwango vya juu ili kuwezesha magari makubwa kusafirisha malighafi na bidhaa za viwandani kwa urahisi wakati wote.

“Kukamilika kwa barabara ya Mkuranga -Kisiju kutaongeza tija kwenye bandari ya kisiju na hivyo kuvutia wawekezaji wa Viwanda na Hotel”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kufanya ukarabati mkubwa kwenye maeneo yote ya barabara na madaraja yalioathiriwa pakubwa na mvua zilizonyesha mwaka huu.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Zilli Kihoko amesema watahakikisha hifadhi za barabara, maeneo ya maegesho na madaraja yanalindwa ili yadumu na kuleta tija kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here