Na Asia Singano, Addis Ababa – Ethiopia
TANZANIA imeshiriki katika kikao cha Kwanza cha Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ugharamiaji kwa Maendeleo Endelevu (Fouth International Conference on Financing for Deveoplopment – FfD4 kilichofanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia huku ikiutaka Umoja wa Mataifa (UN), kujadili upya na kupunguza riba za mikopo inayotolewa kwa nchi mbalimbali.
Akizungumza katika kikao hicho mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban, amesema kutokana na shinikizo (pressure) la madeni inayozikabili nchi mbalimbali kama walivyosema baadhi ya wawakilishi wa nchi hizo, ni vyema Taasisi za Fedha za Kimataifa, zitoe mikopo yenye riba nafuu ili kuziwesha nchi zinazoomba mikopo ziweze kukuza uchumi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
“Tumesisitiza mambo muhimu ambayo katika mkutano wa nne ni muhimu yakazingatiwa ikiwemo upunguzaji wa gharama za ukopaji,’’ amesema Amina.
Amesema kuwa katika kuhakikisha nchi zinaongeza rasilimali za ndani ni wakati sasa wa Umoja wa Mataifa kukamilisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa wa Kodi (International Tax Cooperations) ili kusaidia nchi za Umoja wa Mataifa (UN) kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo.
“Utafutaji wa rasilimali fedha za ndani uende sambamba na framework ambayo watu wa UN waikamilishe, ambayo inaitwa (International Tax Cooperations) hii itatusaidia sana katika kutafuta rasilimali zetu za ndani,” amesema.
Amina ameongeza kuwa kutokana na athari mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kiuchumi ni vyema katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwakani kuhakikisha kuwa zinatengwa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa mazingira na miundombinu ili kupunguza athari za tabia nchi.
“Tumesisitiza kuhusu upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hili ni jambo muhimu na kama tunavyojua sasa hivi tabia nchi inaathiri nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania,” ameongeza.
Katika hatua nyingine Amina amesisitiza kuhusu vijana kupatiwa mikopo kwa ajili ya kufanyia biashara mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi na kusaidia kuleta maendeleo ya nchi.