Kigoma
KADI za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi kuu zijazo bila kujali mabadiliko ya jina la Tume ya Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumza wakati wa ziara aliyoifanya ya kukagua vituo vya kuandikishia wapiga kura leo Julai, 22 2024 katika Halmashuari ya Wilaya ya Kasulu, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ( INEC), Kailima Ramadhan amesema wapiga kura wenye kadi hizo hawahusiki na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Naomba nitoe wito kwa wale ambao kadi zao ni zile zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wanadhania kuwa kubadilika kwa jina la Tume kunasababisha kubadili kadi watambue kuwa kadi zao ni halali kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024,” amesema.
Mkurugenzi huyo wa uchaguzi ambaye kwenye ziara yake aliambatana na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kasulu Vijini, Emmanuel Ladislaus na maafisa wengine waandamizi, alieleza kwamba wenye kadi hizo ambazo zimeharibika, zimepotea au wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine wanahusika kwenye zoezi hilo.
“Nimebaini kuwa wapo wapiga kura wenye kadi za zamani zilizotolewa kabla ya mwaka 2015 (zile za karatasi) hao waje vituoni ili waandikishwe upya kwa kuwa mfumo uliotumika wakati huo ni tofauti na mfumo wa sasa,” amesema.
Kailima amewakumbusha wananchi wa mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi kuwa zimebaki siku tatu kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kukamilika kwenye mikoa yao, hivyo, ni muhimu kujitokeza kwa wingi na kutumia vizuri siku hizo.
Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo umeanza Julai,20 2024 na utafanyika kwa siku saba hadi Julai, 26 2024 ambapo vituo vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.