Home KITAIFA KAMPUNI YA UZALISHAJI UMEME MADOPE KUKABIDHI MIUNDOMBINU KWA TANESCO

KAMPUNI YA UZALISHAJI UMEME MADOPE KUKABIDHI MIUNDOMBINU KWA TANESCO

πŸ“Œ Kapinga asema Serikali itaendelea kushirikiana na wazalishaji binafsi

πŸ“Œ Amuagiza mkandarasi wa umeme vijijini kukamilisha kazi kwa wakati Ludewa

πŸ“Œ Kampuni ya Madope yaishukuru Serikali kwa kuichukua miundombinu hiyo

Njombe

KAMPUNI binafsi ya kuzalisha umeme ya Madope iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe, imefikia makubaliano na Serikali ya kukabidhi miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mara baada ya kusainiwa kwa mkataba.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Nishati, Judithi Kapinga leo Julai 19, 2024 akiwa katika ziara ya kikazi katika Vijiji vya Lubonde na Maweni wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Kapinga amesema kuwa Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa na Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Serikali kwenye uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Amebainisha kuwa, nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wazalishaji binafsi wa umeme nchini.

Akizungumzia usambazaji wa umeme vijijini, Kapinga amesema kuwa Vijiji 151 tu nchi nzima bado havijafikiwa na huduma ya umeme kati ya Vijiji zaidi ya 12,000 na wilayani Ludewa vimebaki Vijiji nane.

Aidha, amemuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme Ludewa ili akamilishe kazi kwa wakati katika Vijiji nane vilivyobaki kati ya Vijiji ishirini vilivyopo Wilayani Ludewa.

Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuendelea kuzalisha umeme mwingi zaidi kutokana na mahitaji kuongezeka kila siku lakini pia uwepo wa miradi inayopeleka umeme nje ya Tanzania.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya Madope Padri Innocent Ngailo amesema Kanisa Katoliki Njombe liliiandikia Serikali barua ya kuomba TANESCO ipokee miundombinu ya umeme inayomilikiwa na Madope na kushukuru kwa Serikali kwa kuitikia ombi hilo.

Padri Innocent Ngailo amebainisha kuwa, Kampuni ya Madope yenyewe itabaki na kazi ya kuzalisha umeme ambao itaiuzia TANESCO.

“Tunawaahidi TANESCO tutashirikiana nao na tutafanya kazi pamoja ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika,”amesema Padri Ngailo

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Njombe, Mhandisi Abdulrahaman Nyenye amewaahidi wananchi wa Vijiji hivyo kuwa TANESCO itafika kutoa elimu na kuwatahadharisha kujiepusha na vishoka.

Mhandisi Nyenye ameongeza kuwa, takribani Vijiji ishirini vilivyokuwa vinahudumiwa na Kampuni ya Madope vitahudumiwa na TANESCO.

Mradi wa madope unamilikiwa na Kanisa Katoliki asilimia 55, Halmashauri ya Ludewa asilimia 45 na Jumuia ya Watumiaji Umeme Mawengi (JUWUMA) asilimia 5

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here