Home KITAIFA JUKWAA LA KILIMO ROUNDTABLE AFRICA LINAWAHIMIZA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KILIMO

JUKWAA LA KILIMO ROUNDTABLE AFRICA LINAWAHIMIZA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KILIMO

Dar es Salaam

JUKWAA linalohimiza ushirikiano, ubunifu, na ukuaji katika sekta ya kilimo (Kilimo Roundtable Africa) limewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya kilimo ndani na nje ya nchi.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 16,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimo Roundtable, Rhoda Mwita, amesema dhamira ya jukwaa hilo katika kukuza sekta ya kilimo endelevu na yenye mafanikio nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, huku akielezea matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa sekta hiyo.

“Tunapaswa kukabiliana na changamoto zilizopo kwa ujasiri, tukionesha kwamba dhamira yetu ni ya muda mrefu na si ya muda mfupi tu. Ninaamini tunaweza kupata suluhu za kudumu na kuonesha uwezo wetu halisi,”amesema.

Amesema sasa ni wakati wa Watanzania kuutumia uwezo mkubwa uliopo katika sekta ya kilimo.

Ameongeza Kuwa mustakabali mzuri kwa vijana wa Kitanzania katika kilimo, na mamilioni ya fursa za kuchangamkia. Kwa msaada unaofaa na ubunifu, wakulima na wafanyabiashara za kilimo zinaweza kuwa mstari wa mbele katika kubadilisha uchumi na kuhakikisha usalama wa chakula na uendelevu kwa kanda nzima.

Rhoda ameisifu Wizara ya Kilimo kwa ajenda ya Uwekezaji 10/30 ya Kuharakisha Ukuaji wa Kilimo Tanzania.

“Mpango wa Uwekezaji wa Ajenda 10/30 na mipango mingine ya serikali katika kilimo imeweka msingi wa mabadiliko ya kilimo nchini Katika Kilimo Roundtable, tunashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mipango hii inatekelezwa.

Tunakusudia kuongeza mauzo ya nje ya mazao ya kilimo na kuunda fursa mpya kwa mazao ya thamani ya juu ambayo yanaweza kuwafaidisha wakulima, wafanyabiashara, na taifa kwa ujumla,”ameeleza


“Ajenda ya Uwekezaji 10/30 ilizinduliwa wiki iliyopita katika Mazungumzo na Warsha ya Wadau wa Mifumo ya Chakula Tanzania iliyoandaliwa kwa ushirikiano na AGRA”,amesema.

Akizungumzia Mtoko huo wa Kwanza wa Wadau wa Kilimo (1st Kilimo Roundtable Gala), utakaofanyika Dodoma wakati wa maadhimisho ya Nane Nane, amesema, “Gala ya kwanza ya mwaka huu, itakayohamasisha Ushirikiano, Ubunifu, na Ukuaji ili kuisukuma Tanzania kulisha Afrika na Ulimwengu pia,inalenga kuitangaza sekta ya kilimo ya Tanzania kimataifa na kukuza ukuaji endelevu.

“Gala itahusisha wadau wote katika mnyororo wa thamani wa kilimo, wakiwemo wakulima, biashara za kilimo, watunga sera, wawekezaji, na wabunifu, ili kuja pamoja na kushirikiana. Kwa kuonyesha uwezo wa kilimo cha Tanzania, kukuza uwekezaji na ushirikiano, kukuza mbinu endelevu, na kuwawezesha wakulima wadogo, gala inalenga kufungua uwezo mkubwa wa kilimo wa taifa hili”,Amesema na kuongeza

“Pamoja, tunaweza kufikia mafanikio kupitia ushirikiano, ubunifu, na dhamira thabiti. Kilimo Roundtable ni jukwaa letu, nafasi yetu ya kuunganishwa, kujifunza, na kuhamasishana. Ni mahali ambapo wakulima wanashiriki hekima yao, wabunifu wanaonyesha ubunifu wao, na watunga sera wanatengeneza mazingira yanayounga mkono ukuaji wa kilimo.”Amesema.

Aidha Washiriki wanatarajia shughuli na fursa mbalimbali katika Gala ya Mwaka ya Kilimo Roundtable. Mambo muhimu ni pamoja na Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane, hotuba za ufunguzi na majadiliano ya paneli, vipindi vya kuunganisha biashara kwa biashara, warsha za kujenga uwezo, burudani za kitamaduni na vyakula.

Amesena Mtoko huo wa Kwanza wa Wadau wa Kilimo unalenga kufikia malengo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kuonyesha uwezo wa kilimo cha Tanzania, kukuza uwekezaji na ushirikiano, kukuza kilimo endelevu, kuwawezesha wakulima wadogo, kuwezesha mazungumzo ya sera, kuzindua taasisi ya Kilimo Roundtable, na kuongeza uelewa wa afya ya akili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here