Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini (TAWA ),Meja Jenerali(Mstaafu) Hamis Semfuko amewahimiza watanzania kuchangamkia fursa za ufugaji wa wanyamapori zinazopatikana katika Taasisi ya TAWA.
Ameyasema hayo Julai 13, 2024 alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Katika Maonesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ambayo kwa Mwaka 2024 leo yamefikia tamati.
“Sehemu kama Afrika ya Kusini ufugaji wa wanyamapori ni mkubwa sana, kwahiyo mimi natoa rai kwa wananchi hasa watanzania kuingia katika biashara hiyo ya ufugaji wa wanyamapori,” amesema.
Aidha Meja Jenarali (Mstaafu) Semfuko amesema ili watanzania waweze kupata kitoweo cha nyamapori kwa urahisi wanapaswa kuingia katika biashara ya ufugaji wa wanyamapori na kwakufanya hivyo wataziwezesha bucha za wanyamapori kufanya kazi vizuri.
Semfuko amesema TAWA ina mipango mingi ya kuhakikisha inapata wawekezaji wakubwa na wadogo ili wawekeze katika maeneo mbalimbali inayoyasimamia kama vile kuwekeza katika mahoteli, vitalu vya uwindaji wa kitalii na ranchi za wanyamapori ili kuongeza idadi ya wanyama hao.
Maonesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yenye kauli mbiu “Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji” yalianza Juni 28, 2024 na kuzinduliwa rasmi Julai 03, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi ambapo leo Julai 13, 2024 yamefungwa na Dk.Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi