Home KITAIFA TRA YAWANOA BODABODA JUU YA ELIMU YA MLIPA KODI.

TRA YAWANOA BODABODA JUU YA ELIMU YA MLIPA KODI.

Na Mwandishi wetu, Dar es salaam.

MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) imetoa semina kwa kundi la Waendesha Pikipiki na Bajaji ili kuwajengea uwezo katika maswala mbalimbali ya kikodi na leseni ili kuimarisha sekta yao inayokuwa kwa kasi.

Akizungumza leo Machi 25 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya Ilala, Edward Mpogolo wakati akifungua semina hiyo ya Elimu kwa Mlipakodi ilioandaliwa na TRA kwa viongozi wa mashirikisho ya waendesha vyombo vya moto ambapo amewapongeza TRA kwa kuandaa semina hiyo ambayo inalenga kutoa chachu kwa kundi hilo juu ya ulipaji pia itaongeza kasi ya mahusiano baina yao na kutokukimbiana kama maadui.

Amewataka viongozi wa makundi ya Bodaboda waliofika katika semina hiyo na kupatiwa mafunzo hayo wakawe mabalozi Kwa wengi. Pia amesisitiza kuwa Serikali inaitambua kazi ya bodaboda na bajaji kuwa ni kazi kama zilivyo zingine hivyo Serikali itaendela kuthamini mchango wao katika kuleta maendeleo na ajila.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano TRA, Hadson Kamoga amesema mafunzo hayo yamehusisha viongozi wa waendesha bodaboda na bajaji ambao ni watu muhimu na wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuendesha uchumi wa miji mikubwa Kama Dar es salaam na mingineyo.

Aidha amebainisha moja ya watakayofundishwa bodaboda hao kuwa ni pamoja na umiliki wa chombo wanachokitumia hususani kwa wale wanaopewa vyombo vya mikataba.

” Tumegundua kuna changamoto ya kutumia chombo ambacho hakina umiliki wake yeye, chombo ni cha kwake lakini tangu alipokabidhiwa baada ya mkataba hajafanya uhamishaji wa umiliki ambapo kadi inasoma jina lingine lakini chombo ana miliki yeye kwahiyo inapotokea changamoto anashindwa kupata haki yake.

“Lakini pia suala la leseni utakuta kuna changamoto waendesha bodaboda na bajaji hawaoni umuhimu wa kuwa na leseni. Na pia wanatakiwa kutambua kuwa kodi zipo kisheria na ni sehemu ya maendeleo, ingawa tumegundua sio kwamba hawataki kulipa kodi, ni kutokana na kutokuwa na elimu,” amesema Kamoga.

Akizungumza kwa niaba ya Bodaboda Mwenyekiti wa bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba ameishakuru TRA kwa elimu hiyo pia amewaomba zoezi hilo kuwa endelevu.

“Tunaishukuru TRA kwa elimu hii ya mlipakodi, tunawaomba isiwe ndo mwisho, elimu hii inatakiwa kuendelea kila mahali, hii itaondoa manung’uniko ili nchi yetu iweze kusonga mbele,” amesema Kagomba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here