Morogoro
WAZIRI wa Maliasili na Utalii MhLAngellah Kairuki ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za wanyamapori.
Kairuki ametoa pongezi hizo leo Julai 8, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kusikiliza changamoto na kutoa utatuzi ili kuboresha utendaji kazi wa TAWA.
“Nawapongeza TAWA kwa usimamizi mzuri wa rasilimali ya wanyamapori kwa kuzingatia kuwa ni Taasisi ambayo haina muda mrefu tangu kuanzishwa kwake,” amesema.
Vilevile, katika ziara hiyo, Kairuki alipata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa TAWA na alisisitiza kuhusu uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu katika kutimiza majukumu yao ili kuboresha utendaji kazi.
Kwa upande mwingine, akizungumzia kuhusu changamoto ya wanyama wakali na waharibifu iliyowasilishwa na Menejimenti, Kairuki alielekeza kuwa miradi ya ujirani mwema ijikite katika kutatua changamoto hiyo kama vile ujengaji wa vizimba pamoja na utoaji wa vitendea kazi kama pikipiki ili kuweza kupunguza changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi (TAWA) Mabula Misungwi Nyanda alimkaribisha na kumshukuru, Kairuki kwa kutenga muda wake na kuitembelea TAWA na alihaidi utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa.
Awali, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage Kabange alitoa taarifa kuhusu maeneo yanayosimamiwa na TAWA huku akibainisha mafanikio na jitihada zinazofanywa na TAWA katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunata Msoffe, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Maliasili na Utalii, Lucy Saleko.