Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu Tume ya Ushindani Nchini (FCC ), William Erio ametoa rai kwa wananchi wote na wafanyabiashara kufika katika banda lao ili wapate elimu ili waepuke kujishighulisha na bidhaa bandia na vitu vingine ambavyo haviruhusiwa na sheria ya ushindani.
Hayo ameyasema leo julai 3,2024 wakati alipotembelea banda la FCC katika maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa ambapo mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu isemayo ‘Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji’.
“Katika sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022 nchini tupo watanzania zaidi ya milioni 60 hivyo muwekezaji anapokuja nchini anauwakika wa kupata nguvu kazi,”amesema.
Amesema sera nzuri za uwekezaji zilizopo nchini ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji lakini pia upatikanaji wa malighafi na uwepo wa miundombinu kam maji,umeme na usafirishaji vimeweza kuchochea uwekezaji.
Erio amesema kufuatia mazingira mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umepelekea nchi kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji.
Amesema pamoja na mambo mengine jambo linalovutia zaidi uwekezaji na kurahisisha ufanyaji wa biashara ni kuwa na taasisi za usimamizi wa shughuli za kibiashara ambazo zipo imara.
Ameongeza kuwa taasisi zitahakikisha na kusimamia vizuri hakuna mfanyabiashara atakaefanya biashara kwa kutumia mbinu chafu na adaifu wala kufanyabiashara kwa kutumia bidhaa bandia.
“Yote haya yatawezekana kama FCC watafanyakazi yao vizuri pamoja na kuchukua hatua za kusimamia kwani hayo ni moja ya majukumu yao na ndio maana tupo hapa pia kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma,”amesema.
Tunataka wafanyabiashara wafanye biashara za halali ili wananchi wanufaike na biashara hizo lakini serikali ipate mapato na tupo tayari kutoa elimu katika kipindi chote cha maonesho,”amesema.