Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema kuwa tangu kuanza kwa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Juni 28 mwaka huu hadi leo zaidi ya ajira 17,000 zimepatikana na zitaendelea kuwepo mpaka pale yatakapoisha Julai 13, 2024.
Hayo ameyasema leo.Julai 3,2024 jijini Dar es Salaam wakati akieleza vitu vilivyofanyika wakati wa maandalizi ya maoneshi ya 48 ya kimataifa ya Dar es Salaam mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.
Amesema kupitia maonesho hayo watanzania wengi wamefaidika katika sehemu ajira na kwamba yamekuwa ni nyenzo muhimu ya kupunguza uhaba wa dola zisizopungua 433,889 kwa kipindi chote cha maandalizi pamoja na kufanikisha ukusanyaji wa kodi kutoka kwa washiriki.
“Washiriki wote hawa wanalipia kodi kwa serikali, Tantrade tunakuvika pete ya mafanikio Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha unaweka mazingira mazuri na rafiki kufanikisha maonesho haya,” amesema Latifa
Aidha amesema katika kuleta upekee wa maonesho hayo wanamshukuru mdhamini mkuu kwa kuboresha mabanda matatu yenye majina ya viongozi wakuu wastaafu ambayo yameokoa Sh. Bilioni moja ambazo zingetumiwa na mamlaka kukodisha miundombinu wakati wa maonyesho.
“Fedho hizi zimeokolewa kutokana na ufadhili wetu mkuu ambaye ni Kituo cha Kuendeleza Biashara cha Afrika Mashariki (EACLC), fedha hizo sasa zitatumika katika shughuli nyingine,” amesema
Hata hivyo amesema wamezindua rasmi leo program ya sabasaba urithi wetu kwa kwaleta watoto kutoka mikoa mitano ya Tanzania ili kuweza kujifunza kinachofanyika katika maonesho hayo.
“Programu hii inalenga kuwarithisha watoto hawa mambo yanayofanyika sabasaba, wakija na kuona jambo hili linakaa kichwani kwao na wanaweza kuijua sabasaba, wanatengeneza historia kubwa kwa kushuhudia maonesho haya,” amesema