Morogoro
KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Hashil Abdallah amewahimiza waandishi wa habari kupitia kalamu zao na vipaza sauti kusaidia katika kuhakikisha taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zinatiliwa mkazo ili kuwezesha umma wa Watanzania kwa ujumla kuhamasika katika kurasimisha biashara zao ikizingatiwa urasimishaji wa biashara hizo unafanyika kwa njia ya mtandao.
Akizungumza leo Juni 18, 2024 mkoani Morogoro akifungua Mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari wanaoripoti taarifa za biashara kutoka Mkoa wa Dar es Salaam yaliyoandaliwa na BRELA, Dk. Abdallah amesema zipo changamoto nyingi ambazo wananchi wanakabiliana nazo kwenye hatua ya kufikia urasimishaji wa biashara.
“Natambua ukuaji wa teknolojia huweza kuwa kikwazo lakini hatuwezi kusimama wakati dunia inakimbia kutokana na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia. Hivyo, changamoto kama hizi ninyi waandishi ndipo taaluma yenu inapohitajika katika kuwaelimisha, kuwaelekeza na kuwaongoza umma,” amesema Dk. Abdallah.
“Niwaombe ndugu zangu wanahabari, kupitia kalamu zenu na vipaza sauti mtusaidie katika kuhakikisha taarifa za BRELA zinatiliwa mkazo ili kuwezesha umma wa Watanzania kwa ujumla kuhamasika katika kurasimisha biashara zao ukizingatia urasimishaji wa biashara hizo zinafanyika kwa njia ya mtandao,”amesema
Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Dk. Abdallah amebainisha kwamba, ni mategemeo yake kuwa kupitia mafunzo haya waandishi wa habari wataacha kuandika habari kwa mfumo wa mazoea kwasababu watakuwa wanataarifa za kina kuhusu BRELA, lakini pia kwa kupitia mafunzo haya itakuwa ni mwanzo wa kuwaweka karibu na taasisi pindi unapohitaji ufafanuzi wa kina.
Amewaomba uandishi wao uzingatie matumizi mazuri ya lugha, kwa kuwa kila mtu anafahamu kuwa lugha ni kitu chenye uhai na kinaweza kutumika kwenye ubunifu katika uandishi, na wazingatie matumizi mazuri ya rasilimali zote za lugha. Kwamba lugha hutuwezesha kutoa maoni, maelekezo, habari na hisia, hivyo kama ikitumiwa ipasavyo huleta uhai katika taaluma ya mawasiliano.
“Hivyo niwaombe waandishi wa habari, kwa kuwa masuala mengi ya BRELA yamekaa kisheria, waandishi mtumie lugha laini kuwaeleza wananchi ili waweze kufahamu kwa kina. Kwa lugha zenu za kitaalamu za uandishi mtaweza kuvunja vunja lugha pasipo kupotosha umma na mkumbuke kuwa jamii inawategemea katika hili,” amesisitiza.
“Wapo waandishi wa habari wanaweza kuwa na mitazamo tofauti kwa namna wanavyotafsiri sheria za utekelezaji wa majukumu ya BRELA na kupelekea muda mwingine kuandika kichwa cha habari kinachopiga kelele (screaming headline) au kichwa cha habari kinachohukumu (judgemental headline) na kuleta taharuki kwa umma naamini kupitia mafunzo haya mtaelekezana kwa kina yale ambayo yamekuwa kigugumizi kwenu kufuatia tafsiri mbalimbali na kupata majibu ya kina,”amesema.
Amesema anaamini kuwa mafunzo haya yatafungua milango ya kuwa na mafunzo kwa waandishi wa habari katika mikoa mingine kwasababu BRELA inafanya kazi nchi nzima na kila mikoa ina waandishi hasa redio za kijamii ambazo zinasikika hadi ngazi ya kata, ambapo amesema wakiendelea na utaratibu huu wa utoaji mafunzo watapata mabalozi wengi wa kuandika taarifa sahihi taasisi hiyo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema mafunzo hayo yanahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari 44 ambapo waandishi 10 kutoka katika vituo vya runinga, waandishi 11 kutoka vituo vya redio, waandishi 12 kutoka kwenye vituo vya habari vinavyochapisha magazeti na waandishi 11 wanaoandikia kupitia mitandao ya kijamii kwa jina maarufu blogs. Kwamba waandishi hao wanatoka katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo vya umma na binafsi.
“Sisi BRELA tutawanoa mambo mbalimbali yahusuyo taasisi kwa muda wa siku nne kuanzia leo tarehe 18 Juni, 2024 hadi tarehe 21 Juni, 2024. Natambua kuwa kwa upana wa majukumu ya BRELA siku hizi nne haziwezi kutosha ila tutawapitisha katika mambo ya msingi na ni kuahidi huu utakuwa ni mwanzo wa safari ya mahusiano yetu katika kuwajengea uwezo na pia kufanya kazi kwa ukaribu pamoja nao,” amesema Nyaisa.
Nyaisa amesema uekelezaji na ufanikishaji wa majukumu ya BRELA yanaongozwa kupitia mpango wa miaka mitano ya taasisi kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026, kwamba Katika malengo manne ya taasisi iliyojiwekea ni kuhakikisha taasisi inakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora na kuwajengea ufahamu wadau katika kuzijua majukumu ya taasisi na kujua namna ya kutumia mifumo yake.
Ameeleza kuwa mbali na utekelezaji wa mpango mkakati, pia taasisi ina mpango mkakati wa mawasiliano wa mwaka 2021/202 hadi 2025/2026 ambapo moja ya mikakati iliyojiwekea ni kujenga mahusiano na wadau wa habari ambao ni wahariri pamoja na waandishi wa habari ila pia kutoa mafunzo pamoja na kuwa na mikutano yenye lengo la kujengana ili kuweza kulisaidia taifa katika ukuaji wa sekta ya biashara.