Home KITAIFA UJUMBE KUTOKA ZANZIBAR KUJIFUNZA SERA YA MADINI TANZANIA BARA

UJUMBE KUTOKA ZANZIBAR KUJIFUNZA SERA YA MADINI TANZANIA BARA

Dodoma

UJUMBE wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini kutoka Visiwani Zanzibar umekutana na Wizara ya Madini katika Kikao kazi cha kujadili na kutoa maoni kuhusu Sera ya Madini ya Zanzibar.

Kikao kazi hicho kimefanyika Juni 10, 2024 katika ukumbi wa Profesa Abdulkarim Mruma Jijini Dodoma ambapo ujumbe huo umejifunza mambo mbalimbali ikiwemo Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ya Tanzania Bara, kujadili na kukusanya maoni kuhusu Sera ya Madini inayoandaliwa Visiwani humo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amewakaribisha wajumbe kutoka Zanzibar na kuwasihi kuendeleza Mashirikiano yaliyopo baina ya Wizara ya Madini na Taasisi zake pamoja na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine, Mahimbali ameupongeza ujumbe huo kwa maamuzi ya kufika Wizarani hapo ili kujifunza na kupata uelewa kuhusu Sera ya Madini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dk. AbdulRahman Mwanga amesema Sera bora ni ile ambayo inaweza kujibu changamoto zilizopo na inatakiwa iwe Sera ya Kudumu zaidi ya miaka 10.

Ujumbe huo, umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango ambaye ameymwakilisha Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Zanzibar, Mariam Yusuf ameipongeza Wizara ya Madini kwa kukubali kuwapatia uelewa na kutoa maoni kuhusu Sera ya Madini ya Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo umefurahishwa na Sera ya Madini iliyopo Tanzania Bara ambapo Wajumbe hao wameahidi kuiga mfano wa Tanzania Bara katika utengenezaji wa Sera inayotekelezeka.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Madini Fred Matola ameipongeza Wizara hiyo kwa uamuzi wa kuchagua Wizara ya Madini ya Tanzania Bara kujifunza namna bora ya uandaaji wa Sera hiyo.

Aidha, Matola ameeleza kuwa, Sera ya Madini inayoandaliwa inapaswa kwenda mbali zaidi kwa kuhusisha masuala ya uchumi wa bluu kwenye madini chini ya sakafu ya bahari na kuzingatia suala la utafiti wa kina wa madini kwani visiwani humo kunauwezekano wa kuwepo kwa viashiria vya Mafuta na Gesi asilia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here