Na Esther Mnyika,
WAZIRI Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mkopo wa dola za Kimarekani bilioni 2.5 ambao Tanzania imepata kutoka Korea ya Kusini hauna mashariti ya kuweka rehani rasilimali za nchi hasa za asili.
Hayo ameyabainisha leo Juni , 6 Profesa Mkumbo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala ya Uwekezaji wakati wa Ziara Rasmi ya Kiserikali aliyofanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Jijini Seoul, Jamhuri ya Korea kuanzia Mei, 31 hadi Juni, 5 2024.
Amesema taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa wakorea wamewapa bahari na madini kama inavyosambaa pia mkopo huo unafaida kubwa kwa nchi.
“Kuna hili linasambaa mtaandaoni kwamba tumechukua mkopo dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa kubadilishana na kugawia bahari na madini yetu kwanza huu sio mkopo wa kwanza kutokea mataifa mbalimbali duniani na hakuna mkopo hata mmoja ambao tumewahi kupokea kwa maana ya kuweka rehani rasilimali zetu hasa za asili haupo,”amesema Profesa Kitila.
Ameeleza kuwa pia sio mkopo wa kwanza kutoka Korea huo ni mpango wa pili walikopa bilioni 1 na mwaka huu bilioni 2 ikijumuisha na ule waliobeba inakuwa bilioni 2.5.
“Kwanza kukopa ni muhimu kwasababu moja ya nyenzo za kujenga uchumi wetu, kujenga uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi wake muhimu tu ni kwamba unapokea kupeleka wapi na mashariti gani,”amesema.
Profesa Kitila Amefafanua amesema kipaumbele chao ni kuchukua mkopo wenye nafuu na kwenda kwenye sekta za uzalishaji hawakupi kwenda kununua magari na kulipa mishahara huo mkopo ni wa miaka 40 na riba yake ni asilimia 0.01 na wanaanza kulipa mwaka wa 26 hivyo ndo mashariti yaliyosemwa.
Aidha amesema katika ziara hiyo wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo kuvutia uwekezaji kutoka Korea na msimamo wa kisera Tanzania kuwavutia wawekezaji kuja nchini.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Korea wamepiga hatua katika sekta ya habari na teknolojia miundombinu hivyo wamejifunza yale waliofanya na walikutana na wabunifu wa biashara changa.
Amesema mchakato wa Tanzania kuwa na setelaiti yake yenyewe unaendelea vizuri endapo mchakato huo utakamilika utasaidia kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
“Mashirikiano kati ya Tanzania na Korea kuwapa mkopo wa kujenga chuo cha TEHAMA dola za kimarekani laki sita na kufanya upembuzi yakinifu,” amesema.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji amesema nchi zilizoendelea kupeleka bidhaa kwa nchi zilizoendelea hivyo wazalishe bidhaa za viwango ziweze kuingia duniania.
“Changamoto kubwa ya viwango vya bidhaa tunazozalisha za viwango vipi?hivyo watanzania tujifunze kutoka Korea kuna kampuni zinakuja kuwekeza tuwe tayari kujifunza na teknolojia yao tuweze kusafiri pamoja,”amesema.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,January Makamba amesema ziara hiyo ya Rais Samia ni moja ya ushirikiano wa kimataifa wa kimaendeleo baina ya nchi ya Tanzania na Korea.
”Viongozi wanaposafiri na Tanzania kuingia katika mazungumzo na nchi nyingine ni katika kutekeleza sera ya nchi ya mambo ya nje ambayo inaelekeza hivyo,”amesema.
Amesema dunia ya sasa ni ya ushindani na ushirikiano,hivyo nchi zimekuwa zinashindana kwa kuvutia mitaji,kutafuta masoko,kupata maarifa ya maendeleo na kutatua baadhi ya changamoto za kidunia zinahitaji majadiliano ili kuzitatua ikiwemo masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
”Maarifa za viongozi lazima yaweze mambo yote mawili ushirikiano na ushindani na katika kuyapata yote lazima kutafuta washirika wa kushirikiana nao na rafiki wa kweli wa kuweza kuhimiri ushindani na kupata maarifa ya kutimiza maendeleo ya nchi,”amesema.
Ameongeza kuwa dunia ya sasa ilipofikia sio ya kukaa ndani ya mipaka yako bila kutoka nje ya mipaka na kuzungumza na dunia ambayo inauwezo wa kusaidia kutimiza maendeleo ya ndani.
”Kwenye dunia ukijifunguia na kusema hutaki kuzungumza na mtu hata maendeleo ya ndani hayawezi kutimi,”amesema.