Home KITAIFA MAKAMU WA RAIS ,  AITAKA  WIZARA YA MALIASILI KUFANYA TAFITI ZA KUZUIA...

MAKAMU WA RAIS ,  AITAKA  WIZARA YA MALIASILI KUFANYA TAFITI ZA KUZUIA UHARIBIFU WA RASILIMALI ZA MISITU

Na John Bera, SAME 

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango ameitaka  Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake  kushirikiana na Taasisi zingine zinazohusika katika mnyororo wa thamani wa rasilimali za misitu kufanya tafiti za namna ya kupata  teknolojia za kisasa ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Akizungumza leo  Machi 21 katika  Maadhimisho ya Siku Ya Misitu Duniani na Upandaji wa Miti Kitaifa yaliyofanyika katika wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, Dk. Mpango amesema sekta ya Misitu nchini Tanzania bado inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo uharibifu mkubwa wa maeneo ya Hifadhi, hali inayochochea mabadiliko ya tabia nchi.

 Amesema matumizi ya nishati chafu (kuni) hapa nchini imeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha ukataji holela wa miti na uharibifu wa Hifadhi za misitu, changamoto ambayo inabidi kukabiliwa haraka iwezekanavyo.

“Takwimu zinaonyesha kuwa, katika kila kaya 10 nchini Tanzania, kaya 9 zinatumia nishati ya kuni na mkaa, hii ni changamoto kubwa ambayo lazima wizara husika ishirikiane na Taasisi zake katika kuikabili,” amrsema Dk.Mpango. 

Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, TAMISEMI, Chuo cha Olmotonyi , Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana kwa dhati na wadau wengine  katika kubuni teknolijia ya kisasa itakayosaidia katika kudhibiti uharibifu wa rasilimali za misitu nchini Tanzania.

“Tafiti na teknolojia hizo ni lazima zilenge katika jitihada za kuvumbua nishati mbadala nyepesi na rafiki, lakini pia, tunahitaji kuwa na teknolojia rafiki itakayosaidia zao la tumbaku kukaushwa bila uharibifu wa mazingira,” ameagiza Dk. Mpango.

Makamu wa Rais amezitaka Wilaya na Halmashauri zote nchini kutenga maeneo mengi ili kuruhusu miti kupandwa kwa wingi zaidi, huku akiwaelekeza Wakurugenzi wa Majiji yote hapa nchini kuanzisha bustani nzuri za miti kwa ajili ya mapunziko na mazoezi.

Awali akimkaribisha  mgeni rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki  amesema kuwa Sekta  ya Misitu inachangia asilimia 3.5 ya pato la Taifa, ikiwa pamoja na asilimia 10 ya ajira kwa Watanzania.

Vilevile, amesema kuwa uhifadhi wa misitu unatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Sekta ya Utalii ambayo inachangia asilimia 17 na asilimia 25 ya fedha za kigeni ambapo jumla ya watalii  1,808,205 walitembelea nchini huku mapato yatokanayo na shughuli za utalii yalifikia dola za Marekani 3.4.

Waziri Kairuki amesema dhumuni la Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa, pamoja na mambo mengine ni kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa upandaji na utunzaji miti, na kuongeza, kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ya ‘Misitu na Ubunifu’ kauli inaonyesha dhamira njema ya Serikali katika kukuza sekta ya misitu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ni siku muhimu sana kwa Taifa na wakazi wa Kilimanjaro, na Wilaya ya Same na Taifa zima kwa ujumla.

Amesema hadi sasa Mkoa wa Kilimanjaro umefanikiwa kupanda zaidi ya miti milioni 8, na kwamba wameweka mikakati mbalimbali endelevu ya kuhakikisha miti hiyo inatunzwa vyema kwa  kuwachukulia hatua kali za kisheria dhidi ya wafugaji wenye tabia ya kulisha mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here