Home KITAIFA JELA MIAKA 50 KWA KUBAKA NA UTAKATISHAJI WA FEDHA

JELA MIAKA 50 KWA KUBAKA NA UTAKATISHAJI WA FEDHA

Lindi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Lindi, imewahukumu kwenda jela miaka 30 kwa kosa la ubakaji na miaka 20 kwa kosa la utakatishaji fedha pamoja na kulipa fedha Sh milioni 35 walizoiba na pia Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa mali zao.

Waliohukumiwa ni Kazil Hamis (Kaftanyi) (43) Mkazi wa Dar es salaam na John Mkondo (Kikwete) (51) mkazi wa Morogoro.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 31, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Consolata Singano wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Awali jopo la mawakili wa serikali likingozwa Wakili Godfrey Mramba alidai kuwa walikuwa na mashahidi 32 na vielelezo 35 vilivyowatia hatiani washtakiwa wote.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka kumi na sita.

Iliendelea kudai kuwa katika shtaka la kwanza la kula njama ya kutenda kosa la wizi washtakiwa wote walikutwa hawana hatia.

Katika shtaka la pili na la tatu ni Kubaka, ilidaiwa kuwa mnamo Machi,1 2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika Wilaya na Mkoa wa Lindi, pasipo na ridhaa washtakiwa waliwabaka Mhanga wa kwanza na wapili(majina yamehifadhiwa) wakiwa katika hali ya kutokujitambua.

Kosa la Nne, tano, sita ni Wizi ilidaiwa kuwa mnamo Machi, 1, 2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika wilaya na mkoa wa Lindi, waliiba Pete ya dhahabu yenye uzito wa gramu 12, yenye thamani ya Tshs 1,800,000/=, Simu moja ya mkononi aina ya Samsung S7 Edge yenye thamani ya shilingi 1,500,000/=, kadi ya benki ya CRDB yenye namba 0152….kadi ya benki ya NMB yenye namba za akaunti 20…..na pesa Sh 300,000/= vitu vyote vikiwa na thamani ya Sh 3,600,000/= mali ya Mhanga wa kwanza. (jina limehifadhiwa).

Pia kati ya Machi mosi, 2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika Wilaya na Mkoa wa Lindi, waliiba saa moja aina Oriflame, yenye thamani ya Tshs 180,000/=, Simu moja ya mkononi aina ya Infinix Hot 11 yenye thamanai ya Tshs 510,000/=, pesa taslimu shilingi 120,000/= vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi 810,000/= mali ya Mhanga wa Pili. (jina limehifadhiwa).

Pia iliendelea kudai kuwa  kati ya Machi mosi, 2022 na Machi, 2 2022 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Lindi na Mtwara, waliiba Fedha taslimu kiasi cha shilingi 35,000,000/= kwenye akaunti ya benki ya CRDB yenye namba 0152… na Akaunti ya benki ya NMB yenye namba za 2010240…. mali ya Mhanga wa kwanza. (jina limehifadhiwa).

Kati ya tarehe zilezile na maeoneo yaleyale washtakiwa kwa pamoja waliiba fedha taslimu kiasi cha Sh120,000/= kwenye laini ya simu ya Tigo namba…..mali ya Mhanga wa Pili. (jina limehifadhiwa).

Kosa la Nane na tisa ni Kughushi, ilidai kuwa Mnamo Machi 2, 2022 eneo Mangaka katika Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, akiwa na nia ya kuhadaa alighushi nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya CRDB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha Sh 4,000,000/= akiaminisha kuwa ni ya kweli na ilikua imejazwa na Mhanga wa kwanza. (jina limehifadhiwa) ilidaiwa kuwa tarehe na maeneo yaleyale washtakiwa wote wakiwa na nia ya kuhadaa walighushi nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha Sh 3,000,000, Wakiaminisha kuwa ni ya kweli na ilikua imejazwa na Mhanga wa kwanza. (jina limehifadhiwa). Sh 3,000,000/= kwa JASMINI ALLY MOKIWA Wakala wa NMB wakiaminisha kuwa ni nyaraka ya kweli ya kutolea kiasi cha fedha kilizojazwa huku wakijua kitendo hicho si cha kweli.

Kosa la kumi ni  kuwasilisha nyaraka ya uongo, mnamo Machi 2 2022 eneo Masasi katika Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, kwa makusudi na wakiwa na nia ya kuhadaa waliwasilisha nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha shilingi 3,000,000/= kwa JASMINI ALLY MOKIWA Wakala wa NMB Wakiaminisha kuwa ni nyaraka ya kweli ya kutolea kiasi cha fedha kilizojazwa huku wakijua kitendo hicho si cha si cha kweli.

Pia iliendelea kudai kuwa eneo na tarehe hiyo hiyo washtakiwa  kwa makusudi na wakiwa na nia ya kuhadaa waliwasilisha nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha Shilingi 4,000,000/= kwa NASSORO SAID SELEMANI wakala wa NMB akiaminisha kuwa ni nyaraka ya kweli ya kutolea kiasi cha fedha kilizojazwa huku akijua kitendo hicho si cha si cha kweli.

Kosa la 12,13,14 ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, ilidaiwa kuwa KAZIL HAMIS @KAFTANYI Mnamo Juni 30, 2022 eneo Tegeta Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es salaam, alitumia laini ya simu yenye namba 07… iliyosajiliwa kwa jina la SHARIFA JONAS HYERA pasipokumjulisha mtoa huduma. Vilevile alitumia laini ya mtu mwingine inayotambulika kwa jina la JACOB ATUPELE MWANDUMBYA pasipokumjulisha mtoa huduma. Pia alitumia laini ya simu yenye usajili wa PAULINA ATHANAS MAGANGA pasipokumjulisha mtoa huduma.

Katika Kosa la kumi na Tano, Kutakatisha fedha, ilidaiwa kuwa  kabla au baada ya Juni 30, 2022 eneo lisilofahamika katika Mkoa wa Dar es salaam, kwa nia ya kuficha chanzo halisi alitakatisha fedha kiasi cha Sh millioni 35,000,000/= kwa kununulia gari aina ya Toyota Aphard Na. 548 DZQ huku akifahamu fedha hizo ni mazalia ya uhalifu wa Wizi.

Kosa la kumi na Sita Kutakatisha fedha, ilidaiwa kuwa washtakiwa wote kwa pamoja tarehe tofauti kati ya Machi mosi 2022 na Machi 2,2022  maeneo mbalimbali ya mkoa wa Lindi na Mtwara, walijipatia fedha kiasi cha Sh milioni 35,000,000/=huku wakifahamu fedha hizo ni mazalia ya uhalifu wa Wizi.

Sambamba na hayo Mahakama imeamuru mshtakiwa wa kwanza na wa pili kuwalipa Mhanga wa kwanza na wa Pili fidia ya Shilingi millioni tano kwa kila mmoja. Pia kurudisha kiasi cha Shilingi milioni 35 kwa Mhanga.

Aidha, Magari matatu yametaifishwa na kuwa mali ya Serikali ambayo ni TOYOTA ALPHARD T. 548 DZQ, NISSAN DUALIS T. 141 DWA na TOYOTA IST T. 978 DJD, amri imetolewa ya ushahidi kuthibitisha kuwa Magari hayo yalitokana na zao la uhalifu, vilevile simu na mali zingine walizokutwa nazo washtakiwa zimetaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Pia gari moja TOYOTA IST T531 DVA Mahakama imeamuru lirudishwe kwa mwenyewe (mmiliki) ambaye hakuwa mshtakiwa katika shauli hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here