Home KITAIFA DK. NCHEMBA AZINDUA MFUMO WA KIELETRONIKI WA FORODHA WA JUMUIYA YA AFRIKA...

DK. NCHEMBA AZINDUA MFUMO WA KIELETRONIKI WA FORODHA WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Na Benny Mwaipaja, Arusha

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amewaongoza Mawaziri wa Nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki (EAC e-Tariff Software), utakaorahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kiforodha. 


Uzinduzi huo umefanyika Mei 31 wakati wa Mkutano wa 44 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha.

Dk. Nchemba ameeleza kuwa kupitia Mfumo huo watumiaji watapata taarifa mbalimbali kuhusu viwango vya pamoja vya ushuru wa forodha kwa wadau wanaohusika na masuala ya kiforodha katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.  


Aidha, amesema Mfumo huo umelenga kurahisisha uchakataji na ufuatiliaji wa maombi ya unafuu wa ushuru wa forodha (duty remission) hivyo kupunguza urasimu pamoja na muda wa kupata huduma hizo.


Katika hatua nyingine,Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, aliikumbusha Kenya, kutekeleza matakwa ya Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) ya kuweka maafisa wa forodha wa Kenya nchini Tanzania watakaofanya ukaguzi wa mizigo inayotoka ama kupitia Tanzania kwenda Kenya.

Ameeeleza kuwa Tanzania imetekeleza Matakwa ya Himaya Moja ya Forodha kwa kuweka maafisa Forodha wa Tanzania upande wa Kenya takribani miaka kumi iliyopita lakini Kenya haijafanya hivyo hatua ambayo inaiathiri Tanzania katika ufanyaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili.


Miongoni mwa athari hizo kwa upande wa Tanzania ni pamoja na kuwepo kwa kadhia ya ucheleweshaji wa mizigo inayotoka Tanzania kwenda Kenya kitendo kinachowaongezea wafanyabiashara gharama, kuwapotezea muda pamoja na msongamano katika mipaka ya Tanzania na Kenya ikiwemo Namanga, Holili, Horohoro na Sirari.

Kwa upande wake Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kenya, Peninah Malonza amesema kuwa Nchi yake itatekeleza Matakwa ya Himaya Moja ya Forodha na kuwaweka maafisa wake wa forodha nchini Tanzania ifikapo Julai Mosi mwaka 2024, ili kundoa vikwazo hivyo vya kibiashara.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Forodha, Biashara na Masuala ya Fedha, Annette Mutaawe, amesema kuwa pamoja na mambo mengine, mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa ambapo lengo kuu la kutano huo lilikuwa ni kujadili masuala ya kuimarisha biashara na uwekezaji katika nchi wanachama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here