Home KITAIFA MAGARI YA UMEME SASA RASMI TANZANIA

MAGARI YA UMEME SASA RASMI TANZANIA

šŸ“ŒUzinduzi wa magari ya umeme kuwawezesha wananchi kutumia nishati safi

šŸ“ŒSerikali yaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini

Na Mwandishi wetu,Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amezindua magari yanayotumia mfumo wa umeme ikiwa ni jitihada za Serikali za kuwezesha wananchi kutumia nishati safi nchini.

Uzinduzi wa magari hayo umefanyika leo Mei 30, 2024 jijini Dodoma sanjari na uzinduzi wa Ofisi za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na kituo cha uzalishaji wa umeme wa jua.

“Niwapongeze wadau wetu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa hatua hii, mtakumbuka kwamba Serikali inaendelea kutafuta mbadala wa kuwawezesha wananchi hasa wale walio na uhitaji zaidi wa nishati safiā€, amesema Dk. Biteko.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau wanaoshirikiana na Serikali kutafuta uwezekano wa kuwa na nishati safi ya uhakika ili kufikia malengo ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNDP, Weyinmi Omanuli ameipongeza Serikali kwa hatua zinazoendelea kuelekea kuwawezesha wananchi wake katika nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi.

Amesema kampeni ya Nishati Safi ya kupikia imekuwa kielelezo thabiti cha Serikali kuwajali wananchi wake hususani wale wa kipato cha chini.

Naye, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Cedric Marel amesema Umoja huo una imani kubwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati kuendeleza jitihada za kuwakomboa wananchi kwa kuandaa mazingira wezeshi yanayolenga kuboresha maisha yao.

Akitoa salamu za utangulizi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema hatua ya uzinduzi wa magari yanayotumia umeme ni mwendelezo wa mpango wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

” Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi nchini,”amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here