Na Ramadhani Kissimba na Farida Ramadhani, Nairobi- Kenya
BENKI ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba katika kikao kati ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba, amesema Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofaidika na uwepo wa Benki hiyo, kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya pande hizo mbili.
Dk.Mwamba amesema Benki hiyo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya taasisi za Serikali kama vile Shirika la Nyumba, benki za biashara kama Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na miradi inayotokana na sekta binafsi.
Amesema pamoja na ufadhili wa miradi ya EADB kwa Tanzania Bara, pia mazungumzo yanaendelea kuhusu miradi mingine kwa upande wa Zanzibar hasa miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
“Tunaendelea kuzungumza kuhusu miradi mingine, hususan Zanzibar ambapo tumezungumza kuhusu mradi wa ujenzi wa makazi ambao kwa sasa tutaufuatilia kwa karibu ili kuona unafanikiwa,”amesema Dk. Mwamba.
Dk. Mwamba ameongeza kuwa Benki hiyo imeonesha nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kwa sasa Tanzania ina asilimia 73 za miradi ambayo inatekelezwa na Benki hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Viviene Yeda ametoa wito kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Benki hiyo kutokana na uwiano uliopo katika umiliki wa hisa unatokana na Benki hiyo ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zina hisa sawa.
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ni mshirika wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Standard Charter Bank ambayo inahudumia nchi wanachama sita ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.