Home KITAIFA IGP WAMBURA AWAVISHA NISHANI POLISI 27 WA VYEO MBALIMBALI DAR

IGP WAMBURA AWAVISHA NISHANI POLISI 27 WA VYEO MBALIMBALI DAR

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura amewataka askari Polisi kuelendea kufanya kazi kwa kuzingatia tunu za Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na nidhamu, haki, weledi na uadilifu.

IGP Wambura ameyasema hayo Mei 18, 2024 wakati akiwavisha Nishani Maafisa, Wakaguzi na Askari Polisi 27 wa vyeo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

Aidha, IGP Wambura amesema dhamira ya Jeshi la Polisi ni kuwa na Jeshi bora la kisasa na la mfano wa kuigwa lenye kutoa huduma sahihi na stahili kwa wananchi.

Katika hatua nyingine amewataka askari kutambua namna ambayo serikali imeamua kuboresha Jeshi hilo na hivyo kufanya kazi kwa bidii, weledi, nidhamu, uaminifu na uadilifu.
“Tujiweke katika kutoa huduma zinazolenga kupunguza malalamiko. Pia askari kutenda kama wenye mali katika kutekeleza majukumu ya kila siku,” amesema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, SACP Muliro J. Muliro, kwa niaba ya maafisa, wakaguzi na Askari waliovishwa nishani leo amesema Nishani hizo ni chachu ya kujenga morali kwa askari kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na usahihi.

“Tunashukuru sana kwa nishani hizi kwani Amir Jeshi Mkuu na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura wameona na kutambua mchango wetu,” amesema.

“Sisi tunaahidi kutenda kwa weledi na kuzingatia sheria, haki na kuwatumikia wananchi kwa kuwafanya wanakuwa salama,”ameongeza SACP Muliro.

IGP Wambura amewavisha nishani askari 27 kwa niaba ya Askari 1247 wa Kanda ya Mashariki ikihusisha Mkoa wa Pwani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Mkoa wa Rufiji walitunukiwa nishani hizo na Amir Jeshi Mkuu na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here