Na Sophia Kingimali.
TAASISI ya umoja wa wanawake wa jasiliamali nchini (Secreto Divas)wameandaa kongamano kubwa lenye lengo la kuwakutanisha pamoja wajasiliamali wanawake wakubwa na wa kati ili kupata elimu ya namna ya kuziendea fursa lakini pia jinsi ya kukuza na kuendeleza biashara zao kw kutangaza biashara hizo kwa kuendana na teknolojia(Market Network)
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 17,2024 jijini Dar es salaam muhasisi wa umoja huo SECRETO DIVAS,Vanessah Mwalugala amesema lengo la kongamano hilo ni kumuelimisha mwanamke kiuchumi lakini pia mahusiano na familia.
“Kitendo cha kumuunganisha mwanamke kwenye biashara,ukimsimamia kwenye familia na kumfundisha namna ya kusimamia biashara zake anaweza kufika mbali na sisi Secreto Divas ndio kitu tunakifanya kuhakikisha tunazitangaza biashara zao na kuwafundisha jinsi ya kufanya biashara mtandao ili kuweza kufanya biashara hizo ziweze kufika mbali,”amesema.
Amesema kufuatia juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan za kumuinua mwanamke na uongozi wake kama mwanamke umewasukuma zaidi kuweza kuhakikisha wanamsaidia mwanamke kufikia ndoto zake.
“Kitu chochote anachokisimamia mwanamke kinafika mbali hata katika uongozi kunakuwa na mafanikio makubwa kama mwanamke akiongoza tunaona mfano wa Rais wetu lakini pia spika wa Bunge Dk Tulia Ackson hawa ni kielelezo tosha katika uongozi,”amesema.
Ameongeza kuwa katika kongamano hilo litakalofanyika Juni 9 jijini Dar es salaam mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa umoja wa Wanawake CCM(UWT) mkoa wa Dar es salaam lakini pia litahudhuliwa na wasanii na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo watoa mada ambao watafundisha na kutoa mbinu mbalimbali katika biashara.
“Nitoe rai kwa wanawake wote nchini kuhudhulia kongamano hili sio la kukosa kwa maana wataweza kujifunza na kuweza kuinuka kiuchumi lakini kupata mbinu mbalimbali zitakazowawezesha wao kuboresha biashara zao na kufikia ndoto zao za kuwa wafanyabiashara wakubwa”,Amesema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Secreto Divas Datty Sinkara amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inawafikia wanawake wote nchini ili kuwapa elimu na mbinu mbalimbali katika biashara zao ili waweze kufanikiwa na kufikia malengo yao.
Pia,ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya juni 9,2024 ili kujipatia elimu na fursa zitakazotokana na kongamano hilo.
Naye,Mshauri Mkuu wa Taasisi hiyo Mohammed Chande ametoa rai kwa wanaume wote kuendelea kusapoti juhudi za wanawake kwani wamekuwa na mchango mkubwa kwenye maendelea ya Familia na Taifa kwa ujumla.
Amesema uwepo wa Secreto Divas umekuwa mkombozi kwa mwanamke katika ukombozi wa kiuchumi kupitia biashara zao hivyo wanawake wanapaswa kufuatilia taasisi hiyo lakini pia kuhudhulia kwenye kongamano ili kujifunza zaidi jinsi ya kuboresha biashara zao.
Chande ametoa rai kwa taasisi na mashirika kujitokeza kwa wingi kudhamini kongamano hilo kwani ni fursa nzuri ya kujitangaza lakini pia kuunga mkono juhudi zinazofanywa katika kumkomboa mwanamke kiuchumi.