Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
TUZO za Wanamichezo bora zinatarajiwa kutolewa June 9 Mwaka huu Jijini Dar es salaam katika Ukumbi maarufu wa The Super Dome Masaki huku zikitarajiwa kuwa za tofauti na za kipee ukilinganisha na za miaka iliyopita.
Akizungumza Mei 15 na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Leodgar Tenga amesema tuzo hizo zimeandaliwa mahususi kwaajili ya kutambua mchango,jitihada na umahiri wa wanamichezo kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa BMT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo Profesa Madundo Mtambo amesema kuwa mchakato wa utoaji tuzo unafanyika kwa uwazi, weledi,na umakini mkubwa, vyama na mashirikisho yote ya michezo yamehusishwa katika uteuzi wa wanamichezo bora katika michezo yao.
“Kamati ya usimamizi wa tuzo tayari imepokea mapendekezo hayo, itayachambua na kuchagua wanamichezo wanaostahili kupewa tuzo,”amesema Prof Madundo
Ameongeza kuwa tuzo za mwaka 2023/2024 ni za kipekee na za tofauti na zilizowahi kutolewa awali ambapo vipengele vimeongezeka ambapo mwaka huu kutakuwa na vipengele 16.
“Mabadiliko ya vipengele vya tuzo yamefanyika ili kuendelea kuipa thamani tuzo hizi zinazotolewa pamoja na kuongeza ushindani baina ya wanamichezo ili mwanamichezo anayepewa tuzo awe ni yule ambaye amekuwa na mafanikio zaidi kuliko wanamichezo wengine wote,” amesema Profesa Mtambo.
Ametaja vipengele hivyo kuwa ni mwanamichezo bora wa kiume wa mwaka, Mwanamichezo bora wa kike wa mwaka, Mwanamichezo bora chipukizi wa Kiume, Mwanamichezo bora chipukizi wa Kike, Mwanamichezo bora wa kiume mwenye Ulemavu, Mwanamichezo bora wa kike mwenye Ulemavu.
Pia timu bora ya mwaka (kwa upande wa vilabu),timu Bora ya Mwaka (Timu upande wa timu za Taifa) ,kocha bora wa kiume wa mwaka, Kocha bora wa kike wa Mwaka, Mwanamichezo bora wa Kiume kutoka katika mashindano ya shule, Mwanamichezo bora wa Kike kutoka katika mashindano ya shule, Mwamuzi bora wa kiume wa mwaka, Mwamuzi bora wa kike wa mwaka, Mwanahabari bora za michezo wa mwaka wa kiume na kike.
Aidha ametoa Wito kwa wadau mbalimbali ,taasisi za serikali na binafsi,kampuni na watu binafsi wanaopenda maendeleo ya michezo nchini kujitokeza kuipa nguvu BMT katika kutekeleza jukumu hilo.