Home KIMATAIFA WASTAAFU WAONYWA KUHUSU MATAPELI

WASTAAFU WAONYWA KUHUSU MATAPELI

Na Asia Singano na Chedaiwe Msuya, Morogoro

WIZARA ya Fedha imeendelea kuwakumbusha wastaafu wanaolipwa mafao na Wizara ya Fedha kutojihusisha na utoaji wa fedha  kwa mtu, kama kigezo  cha kusaidiwa kupata mafao yao, Kwakuwa huduma hiyo hutolewa bure.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye pia ni Msemaji wa Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja, wakati akifungua kongamano la Elimu kwa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini liliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa NaneNane mjini Morogoro.

‘’Naomba muwataarifu wastaafu na familia zao hususani wale wanaolipwa na Hazina kuwa Wizara ya Fedha hailipishi gharama zozote kwa mstaafu ili kumlipa mafao yake,’’ amesema  Mwaipaja.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa taarifa za Bajeti Kuu ya Serikali inayotarajiwa kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni, Mwaipaja amesema kuwa wadau hao wa mitandao ya kijamii wana fursa kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu maudhui na nia ya Serikali ya kuwaletea Maendeleo.

Ameongeza kuwa  wanahabari wana jukumu la kutoa taarifa kwa usahihi ili kuepusha upotoshaji wa taarifa.

‘’Jukumu lenu ni kupeleka ujumbe kwa jamii ambao ni sahihi na wakuaminika, tunahitaji  muwaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kukusanya fedha kwa ajili ya bajeti kuu ya Serikali, kuhamasisha watu kuchangia kwenye bajeti ili kuimarisha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo,’’ amesema Mwaipaja.

Kwa upande wake Mhasibu Mwandamizi, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Kitengo cha Pensheni CPA Jenipha  Ntangeki amrsema kuwa huduma za mafao ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha ama HAZINA zinatolewa bure na kuwaasa wastaafu kujiepusha na matapeli wanaowarubuni wawapatie fedha ili wawasaidie kupata mafao yao haraka.

Amesema pia kuwa katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaunda mfumo wa kidigitali.
“wastaafu portal” ambapo mstaafu atapata taarifa zake zote kupitia mtandao na wastaafu wataweza kujihakiki kidigitali’’ amesema CPA Ntangeki.

Ameongeza kuwa wizara ya fedha  inaendelea kutoa elimu kwa wastaafu na wastaafu watarajiwa kwa kuwa kustaafu kunaweza kutokea hata kabla ya miaka husika kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya kiafya hivyo ni vyema watumishi wa Umma kujiandaa kwa ajili ya maisha yao baada ya kustaafu.

‘’Kwani kustaafu ni ghafla? Kustaafu maana yake ni kushindwa kupata kile kipato ambacho umekuwa ukikipata siku zote,’’ amesema CPA Ntangeki.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kongamano hilo hususani Wamiliki na Watendaji Wakuu wa Mitandao ya Kijamii, Mwenyekiti wa Waandishi wa Mitandao ya Kijamii wanaoandika habari za wizara ya fedha,  Mathias Canal ameipongeza Wizara ya Fedha kwa mafunzo yanayotolewa kwenye kongamano hilo kwakuwa yanasaidia kuwaimarisha wanahabari katika tasnia yao.

‘’ Leo tunajifunza mambo mawili  matatu naamini baada ya kumaliza hapa tutakuwa tumefahamu Sera, Mipango na Mikakati ya Wizara ya Fedha na itakuwa imeturahisishia sisi namna ya kuripoti habari zinazohusu masuala ya Fedha, mafao na mirathi,’’ amesema Kanal.

Hii ni mara ya pili kwa Wizara ya Fedha kufanya Kongamano la Elimu kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii hapa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here