Na Mwandishi wetu, Pwani
WANAFUNZI wa shule ya sekondari Zimbwini iliyopo Kibiti Pwani wamepatiwa mafunzo maalum kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania (TAWA ) Kanda Maalum ya Dar es salaam yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na wanyamapori hususani mamba na kiboko.
Akizungumza Mei, 8 2024 wakati wa mafunzo hayo Afisa mhifadhi wa TAWA ,Sanjo Mafuru amesema uamuazi wa kuendesha mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwaelimisha wanafunzi wanaishi katika jamii zinazozunguka maeneo yanayoashiria uwepo wa wanyama pori hao.
Amesema ilikujihami na kujilinda na mamba uvukapo mto au anapopita kwenye maeneo yenye mamba hakikisha una mti au fimbo yenye ncha Kali na iwapo atakuvamia mchome kwenye macho au kichwani kwa kutumia fimbo au mti huo wenye ncha kali.
Sanjo ameongeza kuwa iwapo huna kitu chenye ncha Kali tumia hata vidole vyako kumtoboa mamba kwenye macho yake naye atakuachia.
Naye Afisa TAWA Kanda Maaluumu Dar es salaam,Zawadi Mslunda amewataka Wanafunzi kujiepusha na matembezi ya usiku ili kujilinda na kiboko na mamba ambao wanaweza kuhatarisha maisha yao hususani kipind hiki cha mvua zinapoendelea kunyesha kutokana na uwepo wa mito na vijito ambavyo wanyama hao hupendelea kuweka makazi.
Zawadi amesema mamba na kiboko huwa wakali zaidi wanapokuwa wana watoto wadogo na wakati wa joto tayari kwa kupandishiwa.
Aidha amewataka Wanafunzi hao kujihami kabisa na makundi ya mamba na kiboko hasa wenye watoto.
Pia Zawadi amewataka Wanafunzi hao kutoa taarifa kwa Uongozi wa TAWA kwa namba za simu walizoziacha shuleni hapo ikiwa ni pamoja na kumuwahisha aliyeng’atwa na mamba hospitali kwa matibabu.
Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo wakaishukuru mamlaka hiyo kwa uwezeshaji huo.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Zimbwini, Tabu Kanon ameshukuru kwa mafunzo hayo huku baadhi ya Wanafunzi wa shule hiyo wanavuka mito yenye mamba hivyo elimu hiyo itawasaidia kuwa salama.
Mwanafunzi sekondari ya Zimbwini, Babrah Gunza ameshukuru kwa mafunzo waliyopata na ameahidi kwenda kufundisha Wanafunzi wenzao na Wazazi wao nyumbani.