Home KITAIFA MAFUNZO YA KUWAENDELEZA WATAALAMU WA USANIFU, UHANDISI NA WAKADIRIAJI MAJENGO TANZANIA

MAFUNZO YA KUWAENDELEZA WATAALAMU WA USANIFU, UHANDISI NA WAKADIRIAJI MAJENGO TANZANIA

Na Mwandishi wetu,Zanzibar

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuziimarisha Taasisi za Ujenzi ili kuhakikisha wataalamu wazawa wanakuza taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Miradi inayojengwa na Watanzania.

Hayo yamesemwa leo Mei 8 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba, Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwaendeleza wataalamu wa Usanifu, Uhandisi na Wakadiriaji Majengo Tanzania hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Maonesho Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, Mei 08, 2024.

Amesema serikali zote mbili zimetoa kipaombele kwa wataalamu wa Ujenzi na Makampuni ya ndani ya nchi kupitia Wizara na Taasisi ambazo zimefanya jitihada maalum za kuweka Sera, Sheria na kanuni zenye vigezo rafiki ili kurahisisha maombi ya kazi za ujenzi hapa nchini.

“Tunataka washiriki wa mafunzo haya kuitumia vyema nafasi waliyoipata ili kuweza kupata uwelewa mkubwa na mbinu mbali mbali za ujenzi ikiwemo utumiaji wa njia mbadala ya vyuma hasa Zanzibar ambapo kumekuwa na uhaba mkubwa wa matumizi mali zisizorejesheka kama vile mchanga na nyenginezo,” amesema Abdulla.

Amesema matumaini makubwa ya serikali kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuonesha mbinu za kuhifadhi, kuitunza na kuiendeleza miji ya urithi ambayo inachangia kuongeza pato la Taifa kupitia watalii wanaokuja nchini.

Pia ametoa wito kwa Makampuni na wataalamu wa Ujenzi kuendelea kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuzingatia ubora unaohitajika na muda wa mradi uliopangwa ili iweze kutumika kama ilivyokusudiwa na kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Katibu Mkuu Wizara hiyo Dk. Mngereza Mzee Miraji amesema kufanyika kwa mafunzo haya kunatokana na mashirikiano yaliyopo kwa Pande mbili za Muungano kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wabobevu hasa katika masuala ya kutunza na kuboresha Miji ya Urithi wa dunia.

Dk. Mngereza amesema ushirikiano uliopo katika Sekta za Ujenzi kwa Tanzania Bara na Zanzibar Umesaidia kuimarika kwa Miundombinu ya Barabara na kupelekea kuongezeka kwa Kipato Kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla pamoja na kuimarika kwa huduma za kijamii.

Kwa upande wa Wenyeviti wa Bodi ya Usajili wasanifu, wahandisi na wakadiriaji majengo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamezishauri Serikali kutumia wataalamu wazalendo katika shughuli za ujenzi ili majengo na Miji ya Urithi iweze kuwa bora zaidi.

Wamesema wakati umefikwa kwa serikali kuangalia sheria na miongozo katika masuala ya ujenzi ili kupunguza changamoto ya kujengwa kwa majengo yasiokidhi viwango na ubora na kuendelea kulitia hasara Taifa siku hadi siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here