Na Mwandishi Wetu,Dodoma
MADEREVA bodaboda 145 katika Jiji la Dodoma- wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani awamu ya pili yalioanza Aprili 15 na kukamilika Mei 4 mwaka huu.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Uswisi kwa kuahirikiana na Shirika la Amend Tanzania yamehitimishwa kwa madereva bodaboda hao kupatiwa vyeti vya ushiriki.
Akizungumza mbele ya madereva bodaboda pamoja na wadau wengine wa usalama barabarani Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amewataka madereva hao kuwa mabalozi kwa bodaboda ambao hawajafikiwa na mafunzo hayo.
“Niwasihi madereva wote waliopokea mafunzo haya kuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani katika maeneo yao kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani,”amesema Asma.
Awali Simon Kalolo kutoka shirika la Amend Tanzania amesema katika utekelezaji wa mafunzo hayo Shirika la Amend linashirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, viongozi wa Serikali za mitaa na shirika la Msalaba Mwekundu wakati wa kutoa mafunzo hayo.
Pia amesema kuwa kupitia mradi huo hadi sasa, mradi huu wa usalama barabarani kwa vijana umewafikia madereva wa pikipiki 398 jijini Dodoma.
“Madereva waliohudhuria mafunzo haya wamepatiwa vyeti vya ushiriki pamoja na viakisi mwanga vyenye ujumbe wa usalama barabarani.Awamu ya kwanza ya mafunzo haya, madereva 253 kutoka kata za Jiji la Dodoma wamenufaika,”amesema.