Home KITAIFA TANROADS KUREJESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA LINDI – DAR ES SALAAM

TANROADS KUREJESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA LINDI – DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu, Mtwara

TIMU ya Watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na Wakandarasi wanaendelea na kazi ya kurejesha miundombinu ya Barabara ya Lindi – Dar- es Salaam ambayo imeharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo ameyasema hayo leo Mei, 5 2024 alipotembelea na kukagua uharibifu uliotokea katika eneo la Somanga – Mtama.

Amesema kuwa leo majira ya asubuhi maji yamefurika kwa wingi na kuharibu eneo la takribani mita 80 katika barabara ya Somanga – Mtama na kukata tuta la barabara hiyo eneo la Mikereng’ende umbali wa Kilomita 10 kutokea Somanga uelekeo wa Lindi.

Pia imeleta athari katika eneo la Lingaula umbali wa kilomita 12 kutokea Nangurukulu uelekeo wa Lindi

Amesema kuwa jitihada za serikali zinaendelea kufanywa ili kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo kutokea upande wa Mkoa Pwani na kutokea Lindi.

Mhandisi Zengo ametoa wito kwa Wananchi na Madereva kuendelea kuwa na subira kwani Serikali kupitia TANROADS inaendelea kufanya kila linalowezekana kurejesha miundombinu ya barabara hiyo na kuwezesha Wananchi kupata huduma ya usafiri katika barabara kama kawaida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here