Home KITAIFA BALOZI DK. NCHIMBI KAZI KUBWA ZA SAMIA ZINAIPA CCM UJASIRI

BALOZI DK. NCHIMBI KAZI KUBWA ZA SAMIA ZINAIPA CCM UJASIRI

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, amesema kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndiyo siri na chachu ya chama na viongozi wake katika kuwatumikia wananchi.

Balozi Dk Nchimbi, ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kati yake na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha Burundi, CNDD – FDD, Mhe. Révérien Ndikuriyo, yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar Es Salaam, leo Ijumaa, Mei 3, 2024.

Balozi Dk Nchimbi ameongeza kuwa katika kutekeleza kwa vitendo Falsafa ya 4R ya Rais Dk.Samia na kuwatumikia wananchi waliokipatia dhamana ya kuongoza, CCM kikiwa Chama kiongozi nchini, kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja wenye mshikamano bila kubaguana kwa kuangalia maeneo wanayotoka, dini, kabila wala itikadi za kisiasa.

“Asante kwa pongezi zako za utekelezaji wa ilani ya CCM. Mojawapo ya nguzo za uimara wa CCM ni pamoja na kazi kubwa sana zilizofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka hii mitatu. Zinatupatia ujasiri na jeuri ya kuwa barabarani, kwenda kuzungumza na wananchi kwa sababu tunayo mambo ya kusema na kuonesha. Na wananchi wanatuunga mkono.

“Lakini pia katika uhusiano kati yetu, CCM tunafurahi sana jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Mheshimiwa Évariste Ndayishimiye ni marafiki. Hivyo vyama vyetu ni marafiki, nchi zetu ni rafiki na hata viongozi wetu ni marafiki, ni wajibu wetu sisi tuendelee kuenzi na kulinda uhusiano na ujirani wetu mwema, kwa ajili ya watu wetu wa pande zote mbili,” amesema Balozi Dk Nchimbi.

Kwa upande wake Ndikuriyo amesema CCM na Tanzania kwa ujumla, ni sehemu muhimu kujifunza kwa ajili ya kujiimarisha, hususani wakati huu ambapo Chama cha CNDD – FDD kinaendelea kuisimamia Serikali ya Burundi katika kulinda misingi ya demokrasia inayotokana na utashi wa Warundi.

Katika ujumbe wake, Ndikuriyo aliambatana na
Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Leontine Nzeyimana na maofisa wengine wa Chama cha CNDD – FDD kutoka Burundi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here