Home AFYA WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA FIGO KWA KUJIEPUSHA NA UNYWAJI POMBE KUPITA KIASI NA...

WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA FIGO KWA KUJIEPUSHA NA UNYWAJI POMBE KUPITA KIASI NA MATUMIZI YA TUMBAKU

Na Shomari Binda, Musoma

SERIKALI imetoa ushauri kwa wananchi kutunza figo kwa kujieusha na matumizi ya unywaji pombe kupita kiasi na uvutaji wa tumbaku.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye hutuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Nkoa wa Mara ,Said Mtanda kwenye maadhimisho ya siku ya figo duniani yaliyoadhimishwa kitaifa mkoani Mara.

Akisoma hotuba hiyo kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Mara Kanali mstaafu Maulid Hassan ambaye ni mkuu wa wilaya ya Tarime amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kampeni kupambana na magonjwa ya figo na yale yasiyo ya kuambukiza.

Amesema serikali katika kuhakikisha inapambana na magonjwa hayo elimu kwa wananchi inatakiwa ili kuweza kupata uelewa wa ugonjwa wa figo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Maulid amesema matibabu ya ugonjwa ya figo yana gharama kubwa hivyo ni muhimu kwa wananchi kuchukua hatua za uchunguzi wa afya kwa haraka.

Amesema serikali pia imejikita kutoa huduma za kibingwa ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo figo.

” Wizara ya Afya imejikita kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa figo na kushauri kuachana na matumizi ya pombe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku. Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hadi sasa imetoa mashine 646 za kusafisha figo ili kuwasaidia watanzania,” amesema Kanali Mstaafu Maulid

Naye Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dk.Osmund Dyagura amesema hospitali hiyo pamoja na mambo mengine mkakati ni pamoja na uhamasishaji wa upimaji na kuhamasisha kufanya mazoezi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ambae ni Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk.Zabron Masatu amesema huduma zimekuwa zikiimalishwa na wenye matatizo ya figo sasa wanahudumiwa hapa mkoani ikiwa pamoja na uchujaji wa damu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here