Home KITAIFA UTEKELEZAJI SERA YA JINSIA NA MAENDELEO YA WANAWAKE, WAJASIRIAMALI 675 WAWEZESHWA MASHINE

UTEKELEZAJI SERA YA JINSIA NA MAENDELEO YA WANAWAKE, WAJASIRIAMALI 675 WAWEZESHWA MASHINE

Na Mwandishi wetu, Dar Es Salaam

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amepokea msaada wa Vyerehani 425 na mashine za kutotolesha vifaranga 250 kwa ajili ya wanawake wajasiriamali nchini.

Msaada huo uliotolewa na Serikali ya China, wenye thamani ya shilingi milioni 79 umekabidhiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingian katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Dar es Salaam Aprili 29, 2024.

Akipokea msaada huo, Waziri Dk. Gwajima amesema Tanzania inatambua umuhimu wa Wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi hivyo msaada huo utakuwa chachu kwenye program ya uwezeshaji wanawake kiuchumi inayoongozwa na na Kinara wa Dunia na Taifa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ambapo, itawaongezea ari wanawake kwenye kuongeza uzalishaji na ushonaji wa nguo na uzalishaji wa vifaranga hivyo kuongeza pato na kuchangia uchumi wa Taifa.

“Tukio hili ni muendelezo wa mahusiano mema ya muda mrefu kati ya Tanzania na China. Msaada huu ni chachu kwa wanawake wa Tanzania kuwekeza katika viwanda vidogo na vya kati vya ushonaji na udarizi nguo,” amesema Dk. Gwajima.

Aidha amebainisha kwamba Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 inayotoa kipaumbele kuwezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuondoa ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini, Chen Mingian amebainisha kuwa, kwa kipindi alichofanya kazi Tanzania amejionea Rais Dk.Samia Suluhu Hassan akitilia mkazo masuala yanayohusu wanawake na kushuhudia baadhi ya wanawake wenye uwezo mkubwa.

Ameongeza kuwa Ubalozi wa China hivi umekuwa ukitoa misaada mbalimbali ya kuwanufaisha wanawake kwenye maeneo tofauti nchini kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi, hivyo msaada huo anaamini utawasaidia walengwa kuongeza kipato.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya wanawake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi Mary Chatanda, ameushukuru Ubalozi wa China kwa kuikumbuka CWT kama sehemu ya wanufaika hivyo hawana budi kuendeleza mradi huo kama jukumu la msingi kwa ustawi mkubwa ili kuwa na uchumi imara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here