Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Lawrence Tax, Aprili 22, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Oparesheni za Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa ,Jean Pierre Lacroix, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Jijini Dar es Salaam.
Jean Lacroix aliyeambatana na Meja Jenerali Cheryl Pearce ambaye ni Naibu Mshauri Mkuu wa Masuala ya Ulinzi wa Amani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa alimueleza Waziri wa Ulinzi na JKT utayari wa Umoja wa Mataifa kushirikiana na Tanzania .
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama na amani katika maeneno mbalimbali ambayo Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania linashiriki.
Lacroix ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake wa kutafuta na kuleta Amani katika sehemu mbalimbali duniani. Mkuu huyo wa idara ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa alimuhakikishia Waziri Tax pamoja na Tanzania kwa ujumla utayari wa Umoja wa Mataifa kuendelea kushirikiana na Tanzania
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, amemshukuru Mkuu huyo wa Idara ya Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wa Tanzania katika Ulinzi wa Amani.