Na Mwandishi wetu, Rukwa
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara, vivuko na madaraja katika maeneo mbalimbali mkoani Rukwa ili kuinua shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi William Lameck amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara za wilaya nchini.
Mhandisi Lameck amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA Mkoa wa Rukwa kutoka shilingi bilioni 5.63 hadi kufikia shilingi bilioni 12.3 ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha mtandao wa barabara mkoani humo.
“Barabara kwa kiwango cha changarawe zimeongezeka kutoka kilometa 867.25 hadi kilometa 1,143.05,” alibainisha.
“Tumeongeza mtandao wa barabara za lami na kufanyia matengenezo ya kawaida maeneo korofi jumla ya Kilometa 196.66, ujenzi wa lami Kilometa 0.8 na zege Kilometa 1.55 zitatengenezwa katika Manispaa ya Sumbawanga na Wilaya ya Kalambo na Nkasi.
“Pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe Kilometa 179.5 na ujenzi wa daraja la Kavunja lenye urefu wa mita 39 linalounganisha vijiji vya Kirando, Kazovu na Korongwe wilayani Nkasi lenye thamani ya shilingi bilioni 1.76 ambapo ujenzi wake umekamilika na daraja linatumika.
Amesisitiza daraja hilo limepunguza gharama za usafiri na usafirishaji ambapo hapo awali wananchi walikuwa wanazunguka katika vijiji vya Wilaya ya Kalambo lakini sasa wanatumia daraja hilo bila kuwa na wasiwasi juu ya mali zao na usalama wao.
Mkazi wa Nkasi, Sarafina Mbalamwezi ameipongeza kwa kile inachokifanya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na kukamilika kwa wakati na wananchi kuondokana na changamoto ya barabara.
Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara umeweza kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma mbalimbali ikiwemo ya matibabu.
Amesema hapo awali kulikuwa na changamoto ya barabara kutopitika hasa kipindi cha masika lakini kwa sasa barabara hizo zinapitika muda wote na madaraja korofi yametengenezwa na yote yanatumika.
Mkazi wa Sopa wilayani Kalambo, Amon Kabwe amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu vijijini ili kuhakikisha wananchi wanasafiri na kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahis.