Na Mwandishi wetu,Dodoma
NAIBU Waziri wa Maji,Mhandisi Kundo Mathew ameipongeza Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) kwa mchango wao mkubwa kwenye mapinduzi ya huduma ya maji vijijini.
Mhandisi Kundo amesema hayo leo Aprili 22, 2024 alipotembelea makao makuu ya RUWASA jijijini Dodoma pamoja na mambo mengine aliwataka watendaji wa RUWASA kutochoka kufanya kazi.
“Bila kupepesa macho, hata waliokuwa nje ya sekta ya maji wanajua hali ya huduma ya maji vijijini ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa RUWASA na hali ilivyo hivi sasa, Hongereni sana.
“Sisi sote ni wasaidizi wa Waziri sio mimi peke yangu, kila mmoja akiongeza bidii kwenye eneo lake tutamimiza ndoto za Waziri na hivyo kutimia ndoto za Rais wetu,” amesema.
Mhandisi Kundo ameitaka RUWASA kuongeza bidii na kukamilisha miradi ambayo imebakiza vitu vidogo vidogo ili ikamilike na kuleta matokeo makubwa.
Kwa upande wa dira za maji, ameitaka RUWASA kuwa na mkakati madhubuti wa matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi (pre paid meters) kama ilivyoagizwa.
Amesema ni muhimu kwa RUWASA kuwa na mkakati utakaohakikisha kila mteja mpya anafungiwa dira ya maji ya malipo kabla ya matumizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amemshukuru Naibu Waziri Kundo kwa kutenga muda pamoja na majukumu mazito ya vikao vya bunge vinavyoendelea kuja kuongea na watumishi wa RUWASA.
Tangu kuanzishwa kwake Julai 1, mwaka 2019 jumla ya wananchi 17,416,1111 wa vijijini wamefikiwa na huduma ya maji kwenye maeneo yao.