Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
MKUU wa Jeshi la Polisi Nchi, IGP Camillus Wambura amepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 235.5 kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS Ltd) leo Aprili 20,2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Polisi Iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Msaada huo unajumuisha mashine ya x-ray ya kisasa, vifaa vya maabara, vifaa mbalimbali vya mazoezi tiba na vifaa vya wodini vya kulazia wagonjwa vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi milioni 235,553,90.
IGP. Wambura amesema vifaa hivyo vimefika wakati muafaka ambapo Jeshi la Polisi lipo katika hatua mbalimbali za maboresho ikiwemo kuhakikisha askari wake wanapata huduma bora za afya.
“vifaa tiba hivi vitaendelea kusaidia kupanua wigo wa utoaji huduma katika vituo tiba vyetu kwa watumishi wa Jeshi la Polisi, familia zao na wananchi kwa ujumla,” amesema IGP. Wambura
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya URA SACCOS ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na menejimenti ya Rasilimali Watu, CP. Suzan Kaganda amesema URA SACCOS imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kutoka na ziada inayopatikana na kuirudisha kwa jamii kwa mujibu wa sheria na kanuni za kiushirikia.
CP. Kaganda amesema kuanzia mwaka 2017 ulipoanza utaratibu huo chama hicho cha ushirika kimeshatoa kwa jamii vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya milioni 581,000,000 lengo ni kupunguza changamoto za kitabibu
“Ushirika unaamini huduma ya Hospitali sio tuu inawanufaisha Askari lakini pia jamii ya watanzania wanaohutumiwa kwenye Hospitali zetu. Hivyo kuleta maana halisi ya kurudisha kwa jamii na kuihudumia kupitia vifaatiba hivyo,”amesema CP. Kaganda.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Anjela Nalimi ameipongeza URA SACCOS pia amesema hii iwe ni chachu kwa vya vingine vya ushirika kuiga mfano huu kwa kutumia sehemu za fedha za ziada kuijali jamii.
Msaada huo wa vifaa tiba unakwenda kutumika katika hospitali ya Kilwa road na zahanati 6 za Polisi ambazo ni Zahanati ya Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar ES Salaam, Zahanati ya shule ya Polisi Moshi, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Mtwara, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Tanga, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Dodoma na Zahanati ya Polisi Mkoa Kaskazini Pemba.