Home KIMATAIFA TANZANIA YANADI FURSA ZA MADINI MKAKATI KOREA KUSINI NA ASIA

TANZANIA YANADI FURSA ZA MADINI MKAKATI KOREA KUSINI NA ASIA

Na Mwandishi wetu, Seoul, Korea Kusini

KATIKA kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Utafiti na Uchimbaji wa Madini Mkakati na Muhimu, Tanzania imepata nafasi ya kunadi fursa zake katika uwekezaji katika shughuli za utafiti wa madini hayo kwenye mkutano wa ‘Madini Muhimu na Mkakati kwa Asia na Africa’ uliofanyika kuanzia Machi 4 hadi 6, 2024 Jijini Seoul, Korea Kusini.

Mkutano huo ulioandaliwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia Taasisi yake ya Jiosayansi na Rasilimali Madini (KIGAM) ulikuwa na lengo la kupata uelewa wa pamoja wa hali halisi ya madini hayo kwenye nchi zilizoalikwa na kujadili namna ya kushirikiana katika kufanya tafiti zitakazolenga kuibua rasilimali hizo lakini pia kuwajengea uwezo Wataalam hususani kwenye teknolojia ya utafiti.

Ujumbe wa Tanzania, uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo akiwa na Wataalam walioambatana naye akiwemo Kamishna wa Madini, Dk. AbdulRahman Mwanga pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dk. Ronald Massawe aliyefanya wasilisho la Tanzania.

Aidha, Katika uwasilishaji wake, Dk. Massawe alifafanua kuhusu jiolojia ya Tanzania sambamba na fursa za madini zinazoambatana nayo. Kuhusu madini muhimu ametoa mifano ya miradi ya madini hayo (kama nickel, REE na graphite) ambayo ipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza uzalishaji.

Vilevile ameelezea jinsi Tanzania ilivyojipanga kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa njia ya kurusha ndege na kuainisha maeneo ambayo Serikali ya Tanzania kupitia GST imeyapa kipaumbele kwenye utafiti huo lakini pia inakaribisha wadau mbalimbali ikiwemo Korea Kusini kuja kushirikiana na GST kufanya tafiti hizo ambazo zitalenga kuibua rasilimali zilizopo kwenye maeneo hayo.

Mkutano huo pia ulitumika kama jukwaa la kutambua juhudi na mafanikio ya Tanzania katika Sekta ya Madini. Serikali ya Korea Kusini, kupitia KIGAM, ilisifu Tanzania kwa mpango wake wa kufanya utafiti wa kina KIGAM pia imeeleza dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania ikifananisha na ushirikiano wake wa utafiti unaoendelea na nchi nyingine za Asia kama Mongolia na Kazakhstan.

Wengine walioshiriki kwa upande wa Tanzania ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini humo, Togolani Mavura na Mshauri wa Mambo ya Uchumi John Masuka.

Mkutano huo ulikuwa ni muhimu kwa Tanzania kwa kunadi utajiri wake kama kiungo muhimu katika Sekta ya Madini duniani na kuweka msingi wa ushirikiano katika utafiti, maendeleo, na uchimbaji wa madini muhimu na mkakati sio tu kwa Tanzania bali kwa bara la Afrika na Asia.

Katika Mkutano huo, Bara la Afrika liliwakilishwa na nchi za Tanzania, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati Bara la Asia liliwakilishwa na nchi za Korea ya Kusini (mwenyeji), Mongolia, Indonesia, Vietnam, Kazakhstan na Uzbekistan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here