Home KIMATAIFA DK. NCHEMBA  TANZANIA IMEPIGA HATUA KIUCHUMI NA KIDEMOKRASIA

DK. NCHEMBA  TANZANIA IMEPIGA HATUA KIUCHUMI NA KIDEMOKRASIA

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu  Nchemba, amelihakikishia Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC) kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya haki za binadamu, utawala bora, demokrasia na usimamizi imara wa uchumi wa nchi.

Dk. Nchemba amesema hayo alipoongoza ujumbe wa Tanzania kukutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa  Shirika hilo, ukiongozwa na Makamu wake wa Rais,  Alicia Mandaville, Jijini Washington D.C nchini Marekani, ambapo pande hizo mbili zilijadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mpango wa kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi, kupitia  ruzuku itakayotolewa na Shirika hilo.


Amesema hatua hiyo si tu kwamba ni utekelezaji wa vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo ili Tanzania iweze kunufaika na mpango huo unaolenga kutoa misaada ya kiufundi, bali ni nia ya dhati ya serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kulinda uhuru wa watu. 

Dk. Nchemba aliihakikishia MCC kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na Serikali ya Marekani katika mpango huo na kuuomba uongozi huo kuuamini mchakato huo na ikiwezekana kuipatia nchi mradi mkubwa wa COMPACT II, utakao iwezesha nchi kupata fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta za usafirishaji, nishati, na maji.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), Chidi Blyeden, aliahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kuanzisha ushirikiano huo wa kimaendeleo kwa kuwa Serikali imepiga hatua kubwa kutimiza vigezo vilivyowekwa ili nchi iweze kunufaika na mpango huo.

Blyeden ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo ambao matokeo yake hapo baadae utaiwezesha Marekani kurejesha mradi wa changamoto za Milenia (MCC-Compact) utakao kuwa na lengo la kusaidia nchi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo. 

Mwezi Desemba mwaka 2023, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ilizichagua Tanzania na Philippines, kama wabia wake katika kuandaa programu za awali (threshold programs) zitakazolenga kufanya mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Bodi hiyo ya MCC ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania na Philippines, kuonesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na rushwa. 

Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ni shirika huru la Serikali ya Marekani linalojielekeza kupunguza umaskini duniani kupitia ukuaji wa kiuchumi, kwa kutoa ruzuku na misaada ya muda maalum kwa nchi zinazokidhi viwango na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na kuheshimu haki za kidemokrasia.

Kupitia Mradi wa Changamoto za Milenia (COMPACT I) uliotekelezwa nchini Tanzania kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, uliiwezesha Tanzania kupata dola za Marekani milioni 698, zilizotumika kutekeleza miradi katika sekta za usafirishaji, nishati na maji.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Tunduma – Sumbawanga, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia, Ujezi wa barabara za Pemba, Tanga hadi Horohoro, Ukanda wa Mtwara, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya usambazaji umeme ukiwemo Mradi wa Umeme Jua mkoani Kigoma pamoja kuyajengea uwezo mashirika ya umeme (TANESCO na ZECO).

Mradi mingine ni upanuzi wa mtambo wa kusukuma maji wa Ruvu Chini ulioongeza kiwango cha uzalishaji maji kutoka lita milioni 180 hadi lita milioni 270 kwa siku na mradi wa usambazaji maji wa mjini Morogoro ambao uliongeza kiwango cha uzalishaji maji kutoka lita milioni 18 hadi milioni 33 kwa siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here