Home KITAIFA SERIKALI IMEWEKA KIPAUMBELE MRADI WA UCHIMBAJI DHAHABU NYANZAGA – MAHIMBALI

SERIKALI IMEWEKA KIPAUMBELE MRADI WA UCHIMBAJI DHAHABU NYANZAGA – MAHIMBALI

📌Asema Rais. Samia anafuatilia maendeleo ya Mradi huo kwa karibu.

Na Mwandishi wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Perseus kutoka nchini Australia ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Jaffer Quartamaine.

Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Ujumbe huo kukutana na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde Ofisini kwake Jijini Dodoma leo Aprili 19, 2024 na kujadili kuhusu uanzishwaji wa Mradi huo.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo wamejadili kuhusu umuhimu wa Mradi wa Uchimbaji Madini ya Dhahabu wa Sotta uliopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza.

Katibu Mkuu Mahimbali ameueleza Ujumbe huo kuhusu matamanio ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuona Mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwamba anafuatilia kwa karibu maendeleo ya Mradi huo.

Mahimbali ameongeza kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kutoa kipaumbele na kusaidia Miradi yote iliyopo katika Sekta ya Madini ikiwemo Mradi huo kwa kuipa umuhimu mkubwa na kutatua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya Perseus Jaffer Quartamaine amesema kuwa Kampuni hiyo imefarijika kuona Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeupa umuhimu mkubwa Mradi huo wa Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu na hivyo kurahisisha mchakato wa mradi katika kutekeleza majukumu yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here