Home KITAIFA RC KUNENGE APOKEA MSAADA WA MAGARI 10 YA JWTZ KWAAJILI YA KUHUDUMIA...

RC KUNENGE APOKEA MSAADA WA MAGARI 10 YA JWTZ KWAAJILI YA KUHUDUMIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI NA KIBITI

Na Scolastica Msewa, Rufiji

MKUU wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amepokea Msaada wa magari 10 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) kwaajili ya shughuli za kusafirisha chakula kwenda kwenye makambi ya Waathirika wa mafuriko ya mto Rufiji katika wilaya za Rufiji na Kibiti.

Akizungumza Aprilii, 18 2024 na Waandishi wa Habari wakati wa kupokea magari hayo huko Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani Kunenge amesema wamepata misaada ya vyakula lakini kulikuwa na changamoto ya usafiri kutokana na miundombinu kuharibiwa na mafuriko yanayoendelea katika wilaya hizo za Rufiji na Kibiti.

Amemshukuru Amiri jeshi Mkuu na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi kwa Msaada huo wa magari kumi na Maafisa 14 miongoni mwao kuna mafundi ambao watasaidia kusambaza chakula kwa walengwa ambao ni Waathirika wa mafuriko ya mto Rufiji.

“Kwasababu mnafahamu tunapata misaada ya vyakula lakini tulikuwa na changamoto ya usafiri kutokana na changamoto ya Barabara lakini magari hayo yatasaidia kupita kwenye maeneo kama hayo,”amesema Kunenge

Amesema magari hayo yatagawanywa kwa wilaya zote mbili zilizoathiriwa na mafuriko hayo ni Wilaya ya Rufiji itapewa magari saba na Kibiti magari matatu kwa kuanzia baadae wanaweza kufanya msawazo kulingana na mahitaji ya wilaya hizo mbili baada ya kufanya tathimini ya kuangalia mahitaji jinsi yalivyo sio lazima yakae upande mmoja bali wataangalia mahitaji jinsi yalivyo na jinsi ya kutumia Msaada huo.

Amekabidhi magari hayo yote 10 kwa Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele kwaniaba ya wilaya yake na Mkuu wa wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo jeshi hilo limeshatoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao wa mafuriko lakini pia wataleta tena boti kwaajili ya kusafirisha vyakula kwenda visiwani na maeneo yanayohitaji usafiri wa kwenye maji.

“Walikwishatuletea vifaa na wao kushiriki moja kwa moja lakini ilibidi tuombe msaada wa ziada baada ya kufanya tathimini tukaona tunahitaji magari ya aina hiyo.

Pamoja na misaada iliyokuja na shughuli za uokozi kwasababu wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na vyombo vingine vya Dola wanashiriki katika uokoaji Sasa hii itatuongezea nguvu na tutakwenda vizuri zaidi,”amesema

Kunenge amelipongeza Jeshi hilo kwa kulinda mipaka ya taifa letu na wakati wa amani kuendelea kuhudumia jamii ya watanzania.

“Kama tunavyofahamu jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ tangu kuundwa kwake linalinda mipaka tya nchi na wakati wa amani linafanya shughuli za kijamii na shughuli hizi za huduma ikiwa ni pamoja na uokoaji pamoja na kupeleka chakula maeneo yanayohusika,”amesema .


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here