Home KITAIFA MGODI WA MAGAMBAZI KUZALISHA KILO 25 ZA DHAHABU KWA MWEZI IFIKAPO AGOSTI...

MGODI WA MAGAMBAZI KUZALISHA KILO 25 ZA DHAHABU KWA MWEZI IFIKAPO AGOSTI 2024

*Unamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100

*Utafiti umebaini uwepo wa mashapo ya dhahabu kiasi cha tani 21.7

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

KAMPUNI ya PMM Tanzania Limited inayomiliki mgodi wa Magambazi imeanza shughuli za uzalishaji madini ya dhahabu ambapo kuanzia Agosti 2024 mgodi huo unatarajiwa kuzalisha kilo 25 za dhahabu kwa mwezi.

Hayo yamebainishwa Aprili, 17 na Mkurugenzi Mtendaji wa PMM Tanzania Limited, Mhandisi Ulimbakisya Spendi baada ya timu ya Wanahabari kutoka Wizara ya Madini kutembelea eneo la mgodi huo uliopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

“Mgodi huu upo katika milima ya Magambazi uligunduliwa na wachimbaji wadogo mnamo mwaka 2003 ambapo mwaka 2007 Kampuni ya Canaco iliomba leseni ya utafiti katika eneo hili na mwaka 2009 iligundulika kwamba kuna dhahabu ambayo inaweza kuzalishwa kwa faida hivyo ikapelekea kuomba leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu,”amesema Mhandisi Spendi.

Amesema baada ya Serikali kuhamasisha uzalishaji katika mgodi huo, Canaco ililazimika kuuza leseni ya mgodi huo mwaka 2020 kwa Kampuni ya PMM ambayo inamilikiwa na watanzania kwa asilimia 100.

Amesema mgodi huo tayari umekwishafanyiwa utafiti na kubaini uwepo wa mashapo ya dhahabu kiasi cha tani 21.7 katika eneo hilo ambapo utafiti bado unaendelea katika mgodi huo.

“Hadi sasa mgodi huu umesaidia ukarabati wa Shule ya Msingi Magambazi, ujenzi wa vyoo katika shule hiii na unaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya ambayo hadi sasa imetumia kiasi cha shilingi milioni 400 hadi kukamilika kwake inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 700 ikiwa ni mchango wa mgodi huu kwa jamii inayozunguka mgodi,”amesema.

Aidha Spendi amesema mgodi wa Magambazi una changamoto kubwa ya umeme ambapo Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeahidi kwamba ifikapo mwezi Juni miundombinu ya umeme itakuwa imefika katika eneo la mgodi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here