Na Mwandishi wetu, Morogoro
BAADHI ya wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wanaotoka katika mazingira magumu wameiomba Serikali kuwapatia bima ya Afya ili kuweza kukabiliana na magojwa yanayowakabili mara kwa mara.
Akizungumza kwa niaba ya watoto hao mmiliki wa kituo cha Raya Islamic Center kilichopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro Raya Subaha Maganga amesema kuwa kutokana watoto kuwa na umri mdogo ambao unashindwa kuhimili magojwa mbalimbali hivyo upo umuhimu wa kupatiwa bima ya Afya.
“Tunafahamu kuwa kulea watoto ni kazi kubwa wadau mbalimbali wanakuja na kutuletea vyakula na vitu mbalimbali lakini suala ya afya ni muhimu sana tunaiomba serikali itusaidie bima kwa watoto hawa kwani hawana msaada na katika kituo hiki tunashindwa kumudu gharama za matibabu kwani watoto wanashambuliwa na magojwa kama tunavyojua watoto wadogo ni rahisi kupatwa na surua,kikojozi,mapunye, minyoo pamoja na tetekuwanga hivyo tukipata bima ni rahisi katika malezi,“amesema.
Wakati suala la bima likionekana kuhitajika kwa watoto wanaolelewa katika vituo vya kulelea watoto wanaotoka mazingira magumu baadhi ya taasisi ikiwemo Hospitali Nanguji iliyopo Manispaa ya Morogoro imeona kunahaja ya kufanya uangalizi wa afya kwa watoto hao ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila katika jamii.