Home KITAIFA wananchi kutembelea banda la Wizara ya Fedha ili kupata elimu.

wananchi kutembelea banda la Wizara ya Fedha ili kupata elimu.

Na Josephine Majura na Asia Singano WF – Dodoma

Wizara ya Fedha imewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kutembelea Banda la Wizara hiyo ili kupata elimu ya fedha, pensheni na majukumu mbalimbali yanayofanywa na Wizara hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Usimamizi Rasilimaliwatu Wizara ya Fedha, Fauzia Nombo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Natu El-maamry Mwamba, kwenye maonesho ya kuelekea kilele cha maadhimiho ya siku ya wanawake duniani yanayofanyika katika viwanja vya Mashujaa, Jijini Dodoma.

Amesema kuwa wanawake wamekua mstari wa mbele kujihusisha na masuala ya fedha ikiwemo vikoba na michezo mbalimbali yanayohusisha fedha hivyo ni vyema wakatembelea Banda hilo ili kujipatia elimu ya masuala ya mikopo na taasisi rasmi zinazokopesha kwa riba nafuu ili kuepuka matapeli na kufirisiwa mali zao pindi watakaposhindwa kurejesha.

“Kuhusu elimu ya pensheni, kumekuwa na utapeli unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii hivyo ni vyema wananchi wakafika bandani hapa ili kupata uelewa wa masuala ya pensheni ikiwemo utaratibu wa kupata pensheni zao bure bila kulipia gharama zozote,”amesisitiza Nombo.

Maonesho hayo ya siku tano yamefunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule.

Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani hufanyika kila ifikapo Machi 8 kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma, yakiwa na kauli mbiu ya ‘’Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii, huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here